Habari

Nasa haiwezi kujiunga na Jubilee kwa sasa – Mudavadi

May 22nd, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi amepuuza uwezekano wa vyama tanzu vya muungano wa Nasa kuungana na Jubilee kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Bw Mudavadi alisema kwamba kulingana na mkataba uliobuni muungano wa Nasa, ni sharti chama kijiondoe kwanza kabla ya kubuni muungano tofauti.

Wiki jana, kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka alinukuliwa akisema kuwa chama chake kingefuata nyayo za Kanu na kuungana na chama cha Jubilee cha Rais Kenyatta.

Kumekuwa na fununu kwamba Bw Mudavadi na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga watashirikishwa katika serikali ya muungano wa kitaifa ambayo Rais Uhuru Kenyatta anapanga kuunda baada ya janga la corona kukabiliwa.

Hata hivyo, Bw Mudavadi alipuuza madai hayo akisema kisheria, vyama vya kisiasa haviwezi kuwa katika miungano miwili kwa wakati mmoja.

“Kama viongozi wa kisiasa tusiwapotoshe Wakenya. Hakuna chama kilicho na uwezo kisheria kutoka Nasa kujiunga na Jubilee kwa sasa. Ni sharti kijiondoe kisheria,” Bw Mudavadi alisema.

Kulingana na mkataba wa Nasa, muungano huo unaweza kuvunjwa vyama vitatu vikijiondoa. Hata hivyo, chama kinaweza kujiondoa kwa kuandikia msajili wa vyama vya kisiasa.

Bw Mudavadi alisema kufikia sasa, hakuna chama kilichojiondoa na kwa hivyo muungano huo ungali imara.

Alitaja madai kwamba anapanga kujiunga na serikali kama propaganda ya kisiasa.

“Kama wanasiasa tunafaa kuwa na sera na kuacha propaganda ambazo zinagawanya Wakenya,” alisema.

Bw Kalonzo alisema chama chake cha Wiper kinaweza kuungana na Jubilee.

“Kwa sasa tuko Nasa na kisheria, hatuwezi kuwa katika miungano mingine. Tunachofanya ni kuunga serikali katika juhudi za kuunganisha Wakenya na kupigana na maovu kama ufisadi na majanga lakini wakati ukifika, tumekubaliana kama chama kubuni miungano kwa lengo ya kuleta nchi pamoja,” alisema.

Makamu huyo wa zamani alisema kuwa Wiper inashauriana na vyama tanzu vya Nasa kuhusu suala hilo.

“Kama Wiper, tunashauriana na washirika wetu ODM, ANC, and Ford-Kenya kuona tunachoweza kufanya. Nchi inafaa kushirikiana wakati huu,” alisema Bw Musyoka.

Akizungumza katika kituo kimoja cha redio nchini Ijumaa asubuhi, Bw Mudavadi alisema kuunga serikali hakumaanishi kukandamiza upinzani.

Wakati huo huo, alilaani ufurashaji wa watu kwa kubomoa makazi yao eneo la Kariobangi na Ruai jijini Nairobi na kuitaka serikali kuwa na utu inapochukua hatua kama hiyo.

“Huu sio wakati wa kufurusha watu kutoka makazi yao. Tunafaa kuweka maslahi ya wananchi mbele ya kila kitu,” alisema.