Nasa ulikuwa muungano wa kusaka uongozi 2017, asema Junet

Nasa ulikuwa muungano wa kusaka uongozi 2017, asema Junet

Na SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Suna Mashariki, Junet Mohammed amesema National Super Alliance (Nasa) ni muungano uliobuniwa kwa minajili ya kusaka uongozi mwaka 2017.

Kiongozi wa ODM, Raila Odinga alitumia mrengo huo akisaidiwa na Bw Kalonzo Musyoka (Wiper) kama mgombea mwenza kuwania urais.

Vinara wengine katika muungano huo na ambao umesambaratika ni Mabw Musalia Mudavadi (ANC), Moses Wetangula (Ford-Kenya), na aliyekuwa gavana wa Bomet, Isaack Ruto (Chama Cha Mashinani).

Huku vinara hao wakilalamikia kuhadaiwa na Bw Raila kwa kile wanadai “amekiuka mkataba uliokuwepo”, Bw Junnet amesema Nasa ilianzishwa ili kusaka uongozi.

Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa Raila Odinga, alisema kwa kuwa malengo yaliyowekwa hayakuafikika kiongozi wa ODM hayapaswi kulaumiwa.

“Ningetaka kuweka wazi kuwa Nasa ilizinduliwa ili kuwania urais 2017, japo hatukutwaa serikali. Kwa nini baadhi ya watu walalamike ati walihadaiwa?” Junet akahoji akizungumza jijini Nairobi.

Akitetea Bw Raila, alisema maagano yanayosemekana yangetekelezwa endapo Nasa ingeingia Ikulu.

Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake, Dkt William Ruto waliowania kuhifadhi nyadhifa zao kwa tiketi ya Jubilee waliibuka kidedea katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8.

Ushindi wao hata hivyo ulifutiliwa mbali na mahakama ya juu zaidi baada ya Nasa kuwasilisha kesi ya kuupinga, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ikaandaa marudio Oktoba 26, 2017.

Nasa haikushiriki zoezi hilo, ikishinikiza IEBC kufanyiwa mageuzi.

Mabw Mudavadi, Kalonzo, Wetangula na kiongozi wa KANU, Gideon Moi wameungana kupitia One Kenya Alliance (OKA), kufuatia mchakato mzima kuwania urais 2022.

Muungano huo hata hivyo haujatangaza ni nani atakayepeperusha bendera ya urais, vinara wake wakimtaka kiongozi wa ODM kuunga mkono nia yao “kama njia ya kurejesha mkono kutokana na ukarimu wao 2017”.

Bw Raila wiki iliyopita kupitia kongamano la kitaifa la vuguvugu la Azimio la Umoja, alitangaza rasmi kwamba atakuwa debeni 2022 kuwania urais.

Wandani wa Waziri huyo Mkuu wa zamani wamekuwa wakiitaka OKA kushirikiana naye katika azma yake kugombea urais.

“Na kwa sababu 2017 hatukutwaa serikali, si waje tushirikiane mwaka ujao,” Junet akasema.

Kinara huyo wa ODM na ambaye amekuwa akishirikiana sako kwa bako na Rais Kenyatta baada ya mapatano kati yao mnamo Machi 2018, amekuwa akiendeleza mikutano ya umma maeneo mbalimbali nchini, kutafuta kura kuingia Ikulu 2022.

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Serikali ifadhili mpango wa kushauri...

‘Taste of Nairobi’ yatoa fursa ya kipekee...

T L