Nasa sinaswi tena

Nasa sinaswi tena

Na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa Chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, amepuuzilia mbali mpango wa wenzake Raila Odinga (ODM) na Kalonzo Musyoka (Wiper) kufufua muungano wa National Super Alliance (NASA).

Mabw Odinga na Musyoka mnamo Ijumaa wakati wa mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Kibwezi, Kalembe Ndile, Kaunti ya Makueni, walidokeza mpango wa kufufua muungano huo kwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Hata hivyo, Bw Mudavadi ambaye ni mmoja wa vinara wa NASA, jana alisema Bw Odinga haaminiki kwa hivyo hatajiunga na muungano huo tena.

“Ninataka Wakenya wajue kwamba kuna ukosefu mkubwa wa uaminifu katika muungano wa NASA ambao hauwezi kurekebishwa. Sisi tunataka kwenda mbele. Tuliunda NASA lakini ukweli usemwe, hakuna uaminifu. Kwa hivyo kama unataka kuturudisha huko na hutaki kukubali kuwa hakuna uaminifu unatarajia tukuamini vipi ukisema unataka muungano nasi? Tuambie watu ukweli,” akasema katika ibada ya Kanisa la Pentecostal Assemblies of God, Likoni, Kaunti ya Mombasa.

Misukosuko katika muungano wa NASA ilianza wakati Bw Odinga alipokula kiapo kuwa ‘rais wa wananchi’ katika uwanja wa Uhuru Park jijini Nairobi mwaka wa 2018, na muungano huo ukaporomoka wakati kiongozi huyo wa ODM alipotangaza muafaka wa maelewano (handisheki) na Rais Uhuru Kenyatta baadaye mwaka huo huo.

Baada ya kiapo hicho tatanishi, viongozi wa ODM walilaumu vinara wenza wa NASA kwa kukataa kusimama na Bw Odinga. Baada ya handisheki, vinara hao wakamlaumu Bw Odinga kwa usaliti alipoungana na Rais Kenyatta bila kuwafahamisha.

Kulingana na Bw Mudavadi, ukosefu wa uaminifu ulionekana wazi wakati vyama tanzu viliponyimwa pesa na pia wakati wanachama walipoanza kufurushwa kutoka kwenye kamati za bunge.

Kwa muda mrefu, vyama tanzu vya muungano huo vimekuwa vikilaumu ODM kwa kukataa kuvigawia fedha ambazo serikali kuu hutoa kwa vyama vikuu vya kisiasa, na hivi majuzi, ANC ililalamika wakati Seneta wa Kakamega, Bw Cleophas Malala alipotimuliwa katika wadhifa wa Naibu Kiongozi wa Wachache katika Seneti.

Katika hotuba yake ambayo alionekana kumshambulia Bw Odinga bila kumtaja moja kwa moja, Bw Mudavadi alisema hana haja ya kushikwa mkono ndipo afaulu kisiasa.

“Ajenda hii inayozungushwa kila mara wanapouliza uko tayari kufanya kazi na fulani, mbona msijiulize kama huyo fulani yuko tayari kufanya kazi na wengine? Msiniletee bwana. Hawa jamaa wanataka kila mara watusukume eti ionekane Musalia hawezi kufanya chochote asipofuata mtu fulani,” akasema.

Bw Mudavadi alikuwa ameandamana na viongozi wa ANC akiwemo Bw Malala na aliyekuwa spika wa bunge la kitaifa, Bw Kenneth Marende, kwa ziara ya siku mbili Pwani.

Awali walikutana na viongozi wa Kiislamu ambapo Bw Mudavadi alipigiwa debe kama kiongozi anayeweza kutatua changamoto zinazokumba nchi ikiwemo mzigo wa madeni ya kitaifa.

Bw Malala alisema watakubali kuingia katika muungano iwapo tu Bw Mudavadi ndiye atakayepeperusha bendera ya urais mwaka 2022.

Haya yamejiri wakati ambapo muungano uliotarajiwa wa Bw Mudavadi, Bw Musyoka, Seneta wa Baringo Gideon Moi ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha KANU, na mwenzake wa Bungoma Moses Wetang’ula anayeongoza Ford-Kenya, kuonekana kuanza kukumbana na vizingiti

You can share this post!

Madereva, wamiliki wa tuk-tuk waandamana Mombasa kwa...

Bidco yazidi kupanua biashara zake barani Afrika