Habari Mseto

Nasa yamkaanga Ruto kushauri muungano huo uvunjwe

December 18th, 2018 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

VIONGOZI wa NASA wamepuuzilia mbali wito wa Naibu wa Rais William Ruto aliyeshauri kuwa vyama tanzu vya muungano huo vivunjwe na kuunda chama kipya kikubwa.

Viongozi wa vyama vya ODM, Amani National Coalition (ANC), Ford-Kenya na Wiper jana walitilia shaka nia ya Bw Ruto huku wakimtaka kutoingilia masuala ya muungano wa NASA.

Alipokuwa akihutubia waumini wa Dayosisi ya Kanisa Katoliki la Kitale katika Uwanja wa Maonyesho ya Kilimo wa Kitale, Jumapili, Bw Ruto alivitaka vyama tanzu vya NASA vivunjiliwe mbali na kuunda chama kipya kikubwa cha upinzani. Alisema umoja wa kitaifa utaafikiwa tu ikiwa patakuwapo na vyama vikubwa vyenye nguvu.

Aliwataka viongozi wa vyama hivyo kuiga mfano wa chama cha Jubilee ambacho kiliundwa baada ya kuvunjilia mbali vyama 12 na kutumiwa na Rais Uhuru Kenyatta kuwania urais.

“Tunafaa kuwa na wasiwasi pale mshindani wetu (Bw Ruto) anapotupatia ushauri wa kuvunja vyama vyetu,” akasema Katibu wa ODM Edwin Sifuna.

Bw Sifuna alisema pendekezo hilo lililotaka vyama vya Wiper, ANC, Ford-Kenya na ODM kuvunjiliwa mbali na kuunda chama kimoja liligonga mwamba kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017.

“Katiba inaruhusu mfumo wa vyama vingi na wala si vyama viwili pekee. Hivyo, wito huo wa Bw Ruto hatuutaki,” akasema kiongozi huyo wa ODM.

Katibu Mkuu wa ANC Barrack Muluka alipuuzilia mbali pendekezo la Bw Ruto akisema kuwa hana lake katika muungano wa NASA. “Bw Ruto anajua wazi kwamba hana chake ndani ya NASA, hivyo maoni yake hayahitajiki,” akasema Bw Muluka.

Katibu Mkuu wa Ford-Kenya Eseli Simiyu alisema Bw Ruto ni mshindani wa muungano wa NASA “hivyo hafai kutueleza namna ya kupanga timu yetu”.

Kulingana na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi Profesa Herman Manyora, Naibu wa Rais anataka Bw Musyoka, Bw Mudavadi na Seneta Wetang’ula kuunda muungano mpya na kumwacha nje Bw Odinga.

Anasema huenda Bw Ruto anataka kuunganisha vyama mbalimbali kama vile Mashinani, Wiper, Ford-Kenya, ANC na hata Muungano Party chake Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana, ili kuvitumia kuingia Ikulu ikiwa atagura Jubilee.

“Bw Ruto anataka viongozi wa NASA; Bw Mudavadi, Bw Musyoka na Bw Wetang’ula waunde chama kimoja bila Bw Odinga. Kiongozi wa ODM akiachwa nje basi itakuwa rahisi kwake kuvuna,” Prof Manyora akaambia Taifa Leo.