NASAHA: Fanya uamuzi wa dhati kuhusu taaluma uitakayo mapema ujifae

NASAHA: Fanya uamuzi wa dhati kuhusu taaluma uitakayo mapema ujifae

Na HENRY MOKUA

DUKA la Mzee Zakayo ni duka la kawaida sana.

Unapolitazama kwa nje unaweza kumwonea imani mzee wa watu – mbona mzee wa umri wake ajishughulishe na duka kama lile na wanawe amewasomesha wakajiunga na taaluma mbalimbali za haja?

Utajiuliza maswali mengi hadi aanzapo kuzungumza nawe; hasa kuihusu biashara yake.

Nimesema naye jana katika kujaribu kujua ni kipi hasa kinachompa mwamko wa kujishughulisha na kazi duni vile – kwa mujibu wa wengi – mimi siamini ipo kazi duni muradi inahitajika kuyafanya maisha ya waja kuwa mepesi hata kwa kiasi kidogo.

Maelezo ya Mzee Zakayo yaliniduwaza…ningeaibika kweli endapo ningekuwa nimeidhalilisha kazi yake.

Kumbe kamera anazozitumia ni ghali vile? Kamera mbili tatu kwa shilingi nusu milioni! Naafadhalisha nusu milioni kuliko laki tano kwa sababu itazua dhana kwamba mzee yule kumbe ni milionea! Lakini si ni kweli…mzee wa watu ni milionea japo huwezi kumkisia vile!

Uamuzi wa dhati (decisiveness) ni jambo muhimu sana maishani.

Mwandishi na hatibu mashuhuri Joyce Meyer anashtakia kwamba ni heri kufanya uamuzi mbaya kuliko kutofanya uamuzi wowote. Anadai kwamba huenda uamuzi mbaya ukawa ni fursa kwako kujifunza na kujiepusha na kosa au lile lililokufika.

Binafsi sidhani kwamba uamuzi mbaya unaoepukika ni hatua ya busara, lakini nakisia mwandishi huyu anasisitiza umuhimu wa kufanya uamuzi wowote uwao kwa wakati badala ya kuhangaika baina ya uteuzi mmoja na mwingine.

Kwako mwanafunzi katika ngazi ya shule ya msingi au ya upili, amua kwa wakati ni taaluma gani utakayoizamia kati ya nyingi unazoziwazia.

Uamuzi wako wa mapema na ya dhati utakuwezesha kuamua kwa wakati hali kadhalika ni masomo yapi utakayohitajika kuyaegemea ili kujiunga na taaluma hiyo ya ndoto yako.

Ikiwa ungependa kabisa kuwa mhandisi na ufanye uamuzi huo mapema, uwezekano mkubwa ni kwamba utazoa alama za haja katika masomo ya msingi ya kukuingiza kwenye kozi hiyo kama vile Hisabati na Fizikia.

Ubaguzi

Katika jamii hii ambapo kazi zimeainishwa, kuthaminiwa na kudhalilishwa kwa msingi wa kipato, usipoufanya uamuzi wako kwa dhati, utaishia kuichukia kazi yako kwani huenda ukajiunga nayo kwa kukosa mbadala.

Ukweli wa mambo hata hivyo ni kwamba hakuna kazi bora kuliko nyingine almuradi kila mmoja ajiunge na taaluma inayowiana na uwezo wake.

Kufanya uamuzi wa dhati kuhusu taaluma uitakayo ni msingi muhimu wa kuanza kuithamini kazi yako mapema – sijawahi kumwona mtu aithaminiye kazi yake akilalamika kwamba haimfai; kuithamini kazi yako ni muhimu mno ila lazima ufanye uamuzi wa dhati kuihusu kwanza ndipo uithamini vilivyo!

Kumbe Mzee Zakayo alianza kujifunza na kujizoesha kupiga picha angali mwanafunzi. Aliamua mapema hiyo kwamba hatajishughulisha na jambo jingine mbali na kupiga picha.

Hakupoteza muda kuangaza angaza macho kuamua ajiunge na kozi gani baada ya kuhitimu masomo ya sekondari. Hapo ndipo uwezo wake ulipomfikisha na akazamia kazi yake.

Nyuma ya duka lake lile anayo ofisi ya kujivunia kwani imepambwa ikapambika. Alinipa fursa kuzitazama baadhi ya picha alizozipiga – za kitambo na za sasa – mbona zinavutia sana!

Mashamba anayo, magari hali kadhalika…nayataja kwa kuwa ni baadhi ya vitambulisho vya fanaka katika jamii nyingi.

Wanawe amewasomesha na bado anayo ari na uwezo wa kuwashughulikia wajukuu wake kuhakikisha kwamba nao wanafanikiwa masomoni na maishani pia.

Ewe mwanafunzi unayesitasita kuamua usomee nini kwa sababu unaona ukijiunga na kozi inayodhalilishwa utachekwa na kupuuzwa, zinduka sasa na kulenga ndipo!

Amua mapema ni kozi gani itakupa mshawasha wa kuamka kila uchao kuwatumikia waja wenzio…kisha fanya mashauriano kuihusu. Je ina faida gani?

Changamoto je? Anza kujishawishi na kujinasibisha mapema nayo kwani ukiithamini italipa bila shaka.

Aidha, utaweza kushindana kwa ari na kujipa nafasi ya haja miongoni mwa washindani wako.

Kila la heri unapofanya uamuzi wa dhati kuhusu ni kipi utakachokisomea baada ya kuhitimu masomo ya msingi na ya sekondari.

You can share this post!

KINA CHA FIKIRA: Ujeuri wa mpapai hujeruhi na udhalili wa...

Serge Aurier ajiunga na Villarreal ya Uhispania