NASAHA: Lengo kuu la kufunga ni kuwawezesha Waislamu kupata ucha-Mungu

NASAHA: Lengo kuu la kufunga ni kuwawezesha Waislamu kupata ucha-Mungu

Na KHAMIS MOHAMED

MWEZI wa Ramadhani ni katika miezi bora katika miezi kumi na miwili ndani ya mwaka mzima. Ndio mwezi ambao Allah amebainisha wazi kheri na neema nyingi zilizomo ndani yake. Pia ni ibaada ambayo walifanya wema waliopita na hata kaumu zilizopita.

Pia ndio mwezi ulioteremshwa Quran. Ndio mwezi Waislamu na Mtume (S.A.W) wamepata ufunguzi wa mji wa Makka baada ya kufukuzwa na kuteswa kwa kulingania dini, ndio mwezi wa pekee ambao Mwenyezi Mungu anatoa rehma kwa waja wake. Anawasamehe dhambi na makosa waliofanya pamoja na kuwatoa katika moto na adhabu iumizayo.

Mfungaji Mpendwa, lengo kuu la sisi kuwekewa ibada ya funga ni tupate kumcha Allah. Kifungu hiki cha maneno kinaeleza hekima kubwa inayofungamana na saumu. Ni desturi ya Qur’an inapotoa amri yenye maana, papo kwa papo inaeleza faida yake ili mtu ajue na atosheke na hekima ya kupewa amri hiyo.

Katika kifungu hicho kusudi la Saumu limeelezwa kuwa ni kupata Taq-waa, yaani, ucha-Mungu. Neno Taq-waa, linatumiwa katika Qur’an kwa maana kuepukana na dhambi, na kufikia utakatifu ulio juu wa mambo ya kiroho.

Uchamungu maana yake ni sifa anayokuwa nayo mtu ambayo inamfanya apate ‘msukumo’ maalum wa kufuata maamrisho yote ya Mwenyezi Mungu na kuacha makatazo yake. Mchamungu huwa anajiepusha na mabaya na anajiweka karibu na kuyafanya yaliyo mema yanayomridhisha Mola wake na wanaadamu wenzake.

Mwenyezi Mungu amesema katika Quran Tukufu: “Enyi Waumini mmefaradhishiwa kufunga kama walivyofaradhishiwa waliokuwa kabla yenu ili muwe wacha-Mungu”.

Faida za uchamungu zipo nyingi tu na kubwa ni kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kumuingiza mja kwenye pepo yake.

Ili kupata pepo ya Mwenyezi Mungu na msamaha wake lazima Muislamu ajipinde sana hususan katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Kadhalika Mwenyezi Mungu anasema kwamba pepo imeandaliwa wachamungu (na moto kwa wanaomuasi). Hivyo, Muislamu anapofanya ibada, kuswali, kufunga, kutoa zaka, kwenda kuhiji na ibada zingine huwa matarajio ni kupata pepo ambayo ni maisha ya milele na siyo kufanya hayo kwa ajili ya kujionesha kwa wanadamu.

Kama mfungaji atafunga ama kumaliza mfungo na hajaacha maasi sambamba na kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu basi kwa mafundisho hayo ajue anafunga kwa mazoea na lile lengo la kufunga ambalo ni kupata uchamungu linakuwa halijatimia kwake.

You can share this post!

Mwanamume amshtaki Magara akidai ni babake

Mwanawe Haji aapishwa useneta katika kikao maalum