NASAHA: Mwandalie mwanao jukwaa la kuyaratibu malengo yake na jinsi atakavyoyaafiki

NASAHA: Mwandalie mwanao jukwaa la kuyaratibu malengo yake na jinsi atakavyoyaafiki

Na HENRY MOKUA

MATUKIO ya awali na mafunzo yatokanayo nayo ni msingi muhimu wa kuyafanya maamuzi ya halafu.

Hii ndiyo hali mara nyingi na kuna kila sababu ya kujiegemeza kwenye historia ili kuibuka na maamuzi mwafaka kuhusu mustakabali.

Hata hivyo, kiasi kilivyo muhimu katika kila jambo, ki muhimu katika hili pia. Nasema hivi kwa sababu wikendi iliyopita nilisimuliwa kisa cha kukatiza tamaa kitokanacho na hali hii. Kwa msingi kwamba mzaliwa wa kwanza alilifanya jambo fulani visivyo akiwa katika umri fulani, mzazi aliamua kumnyima mdogo wake fursa ya kulijaribu jambo lile, akihofia mzaliwa wake wa pili angeshindwa nalo pia.

Mtoto yule alinieleza kwa majuto makubwa ambavyo hajafurahishwa na hali ya kuhofiwa kutomudu majukumu yaliyomshinda mtangulizi wake miaka michache iliyopita. Kuwaziwa kwake kwamba angeyakatiza masomo yake kama mkubwa wake na hivyo kutelekezwa kulimkera kweli. Alishangazwa mbona yeye ni yeye na ndugu yake ni ndugu yake! Wakati mzazi ukidhani umeyafanya yote unavyostahiki kuyafanya unagundua kwamba zipo nyufa zinazopaswa kuzibwa. Ukweli ni kwamba uzoefu wetu na tajriba inayotokana na yaliyofanyika siku za nyuma huyaongoza maamuzi tunayoyafanya kuhusu mustakabali wetu. Pia huweza kuchangia maamuzi yetu ya sasa. Hata hivyo makini ni muhimu kukadiria kiasi cha kufanya vile kwani tukipitiliza tunajikuta pabaya.

Unapofikia pa kumsimanga mtoto kwa kushtakia kwamba hawezi kuzua tofauti; kwamba atashindwa mwenziwe alivyoshindwa, unamtia mtoto mwenyewe katika hatari ya kuyakiuka maelekezo yako. Kwa kuwa inatubidi kujifunza kutokana na matukio hayo ya awali, ni muhimu kufanya vile kwa tahadhari kubwa tusije tukajikwaa.

Pana haja ya kumpa kila mwana fursa ya kuyajaribu anayohisi atayamudu muradi hayakiuki maadili ya mle nyumbani wala kuzua hasara kubwa, kuhatarisha maisha. Kudhihirisha imani uliyo nayo kwa mwanao japo awe mnyonge ndiyo njia hakika ya kumhimiza na kumhamasisha awe bora zaidi. Kauli zitokazo kwenye mtu aliye na mamlaka ulivyo nayo ewe mzazi ni kauli zenye uwezo wa kuyabadilisha maisha ya mwananadamu kabisa kwa njia chanya.

Wazia kuwa na kikao na mwanao na kumpa fursa ya kujieleza. Mruhusu akueleze malengo na matazamio yake. Mhimize akutajie hatua halisi anazonuia kuzichukua ili kuyafikilia malengo hayo. Akionyesha nia ya kuyajaribu yaliyompiku mkubwa wake awali, mpe fursa bila masharti lakini chini ya uangalizi wako wa karibu. Akitaka kuyateua masomo yale yale aliyoyachagua mwenziwe yakambwaga, mpe fursa. Utagundua baadaye kwamba ungeibuka kizingiti maishani mwa mwana huyo kwani ana uwezekano wa kufanya vema kiasi cha kupigiwa mfano.

Nawe mwana jifunze kuwa na subira na uelewa kwamba kila mzazi ana nia njema na mwanawe. Hivyo basi anapokukataza jambo, uwezekano mkubwa ni kwamba makatazo yake ni tahadhari tu ya kukuepusha na kukatizwa tamaa. Ijapo hakuna kanuni inayokataza kufeli, mzazi asingetaka ulijaribu jambo ambalo anashawishika hutalimudu.

Iwapo kikao baina yenu wawili hakitawafikisha kwenye mwafaka ili ukapata fursa ya kulifanya linalostahiki, mtafute mtu atakayewapatanisha kimtazamo ili awe na kikao nanyi msije mkapoteza fursa muhimu ya kuzua mabadiliko nyumbani mwenu, katika eneo lenu, nchini mwenu au hata ulimwenguni.

Ewe mwanafunzi usisahau lakini kwamba ndiwe wa kwanza na wa msingi zaidi kujiamini na kumshawishi kila yeyote kwamba utalimudu zoezi unalonuia kupewa fursa kulitenda.

Hata utakapokatazwa na hata kuzuiwa, kumbuka fursa nyinginge itajitokeza – kwa hivyo usije ukazua mzozo – zidi kujiamini na kuzinoa stadi zako ili kwamba utakapopata fursa katika siku za halafu, utaitumia vilivyo kiasi cha kuyavutia makini hata ya wale waliokuzuia awali.

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Franklin Mukembu

NDIVYO SIVYO: Bandubandu huisha gogo na chovyachovya...