Makala

NASAHA: Ni nini hekima ya Waislamu kulazimika kufunga Ramadhani?

May 6th, 2019 2 min read

NA KHAMIS MOHAMED

WAISLAMU wameingia tena katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Ni mwezi ambao unatoa taswira ya lengo la kuumbwa kwa mwanadamu, ambalo ni kumcha Mwenyezi Mungu.

Hekima inayopatikana katika funga haiishii tu kwenye kiu na njaa, ingawa suala la kuwa na kiu na njaa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu linatosha kupata baraka na kuwa chanzo cha uchaji Mungu.? Katika Quran, amri hii ya kufunga inatangazwa wazi: “Enyi mlio amini! Mmewajibishwa funga, kama walivyowajibishwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kumcha Allah” (2:183).

Katika darsa yetu ya nasaha za Ramadhani hii leo ningependa tujiulize na tutafakari kwa pamoja ni nini hekima ya kufaradhishiwa kufunga?

Katika kubainisha hukumu ya kufaradhishwa na kuwajibishwa kufunga, Qur’ani tukufu imeitaja taqwa na Ucha Mungu kuwa moja ya hekima za kufaradhishwa amali hii ya Kufunga kama vile Quran tukufu. Aya ya 183 ya Suratul Baqarah inasema:

‘’Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama walivyo andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kumchamungu’’.

Swaum ni chuo (shule) ya kumfunza mtu ucha mungu ili pindi swaum inapokwisha mja adumu katika twaa (ibada) ya Allah (S.W) hadi Ramadhani nyingine. Na Ramadhani nyingine tena ajifunze (aongeze) daraja ya ucha mungu zaidi ya aliyokuwa nao, na mwaka mwingine vivyo hivyo hadi yanapomkuta mauti yamkute katika darja ya juu katika ucha mungu.

Je ni nini ucha mungu ambao Allah (S.W) Anaokusudia tuupate kwa kupitia funga? Nini maana ya ucha mungu?

Ucha Mungu (Taqwa) ni kumuogopa Allah (S.W) kwa kujilinda na maasi na kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu (S.W) katika kila nukta ya maisha yake toka anapoamka hadi anapojibwaga kitandani kwa ajili ya kulala tena.

Kumuogopa Allah (S.W) ni kuamini kwamba yupo na anakuona katika kila ufanyalo,hivyo basi unalifanya kwa tahadhari ya hali ya juu ili usije ukamuudhi.

Anasema Sahaba ya mtume Muhammad (S.A.W) Ubay ibn kaab (R.A) alipoulizwa na sayyidna Umar (R.A) juu ya ucha mungu,akamuuliza sayyidna Umar (R.A), je umeshawahi kupita njia iliyo na miba? Akamjibu “ndiyo”. Ubay (R.A) Akamuuliza, “ulifanyaje?” Umar (R.A) Akamwambia “nilipandisha nguo zangu juu na kuzikusanya pamoja na kupita kwa uangalifu mkubwa ili nguo zangu zisijenasa kwenye miba hiyo. Ubay (R.A) Akamwambia na huo ndiyo ucha mungu,kujilinda mja na dhambi za dunia hii,ili aweze kuitimiza safari bila mikwaruzo ya miiba ya dhambi.

Hivyo basi hii ndiyo taqwa,na mwenye hayo yote kwa pamoja, huyo ndiye mcha mungu. Na hii ndiyo sababu ya Allah(S.W) Kutuamrisha kufunga ili tuweze kuyafikia haya, na kuongeza darja ya mambo haya kila mwaka hadi kufikia daraja ya juu katika ucha mungu.

Na kwa kumalizia nakumbuka niliulizwa na ndugu yangu mkristo, Kwani Mwenyezi Mungu hatupendi sisi waislamu , atuamrishe tushinde na njaa (tuache kula na kunywa) mchana kutwa, lengo ikiwa kupata ucha mungu? Je hakuna njia nyingine mbadala ya kupata ucha mungu?

Nikamjibu kuwa funga ni moja ya amali bora kabisa za kumwezesha muumini kudhibiti ghariza za kihayawani na kuhuisha moyo wa uchaji Mungu ndani ya nafsi yake.

Wafasiri wengi wamesema hii inaonyesha hekima ya saumu ambayo ni mazoezi ya mwenye kufunga kuweza kuthibiti nafsi, kuacha matamanio ya haramu na kuwa na kudumu katika twaa na kutenda matendo mema nay a kheri.

Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi.