NASAHA: Nukta muhimu za kuzingatia mitihani ya kitaifa inapojongea

NASAHA: Nukta muhimu za kuzingatia mitihani ya kitaifa inapojongea

Na HENRY MOKUA

SIKU ambayo umekuwa ukiingoja sana, ambayo ulikuwa ukiiona kwa mbali tu miaka minne au minane iliyopita inazidi kujongea.

Katikati ya majuma mawili hivi itakuwa imewadia. Je umejiandaa vipi kuikabili ukijua kwamba umeisubiri sana? Je ujasiri na utulivu wako unazidi kuongezeka au kudidimia? Kumbuka siku chache zilizosalia ndizo zitaamua endapo umewekeza miaka minne au minane iliyopita vilivyo.

Wapo waliojiandaa vilivyo katika kipindi chote hicho lakini wakamaliza visivyo kwa sababu ya uteuzi mmoja mbaya.

Wengine waliotatizika mle katikati, katika siku zao za awali, madarasa au vidato vya awali wamewahi kufanikiwa kiasi cha haja kwa kumaliza vilivyo. Simhimizi yeyote kuzembea ati angoje kumaliza vizuri, kila hatua ni muhimu – na kuichukulia kila mojawapo kwa uzito ndio msingi wa matokeo bora zaidi. Kumaliza kwa makini lakini kuna nafasi muhimu katika jambo lolote la kuthaminiwa. Yapo mambo machache yatakayokuhakikishia ufanisi pamoja na maandalizi yako mazuri.

Jambo la kwanza ni nidhamu. Wajua kwamba kutotia nidhamu maanani kwaweza kukufanyiza usiyoyatarajia? Ndiposa nakuhimiza kwamba uhiari kujiepusha na masuala yote yanayohusiana na utovu wa nidhamu hasa katika kipindi hiki kwani ni rahisi kupoteza miaka minne ya jitihada kwa kuteleza kidogo tu.

Iwapo hujawa mtiifu, jaribu kadri ya uwezo wako kuwatii wote wanaostahiki katika siku chache zilizosalia. Utakapoona ugumu, fanya mashauriano kwa utulivu ili uelekezwe. Kuitwaa sheria mikononi mwako hakutakuzuia tu kufanya mitihani bali pia kukuingiza katika kesi zisizoisha ungali mkembe hivi.

Ijaze akili yako na picha za mustakabali wako mzuri wakati ukifuzu, tuzo utakayojipa au kupewa baada ya kufuzu. Wazia taaluma ya ndoto zako utakayojiunga nayo, nyumba utakayoishi kwayo, kuridhika utakakoridhika kwa kupata matokeo yanayowiana na bidii yako. Hamna hamasa inayoshinda hii kwa kila yeyote atakaye kufanikisha jambo.

Hamasa inayotoka moyoni mwa mtu binafsi yaweza kuyashinda majabali ya maisha. Kwa kujikumbusha maisha mazuri unayoyatarajia baada ya kuupasi mtihani, utapata nguvu mpya ya kuamka mapema, ya kuendelea na maandalizi hata unapokabiliana na vikwazo bayana kabisa. Uone ufanisi wako kama zawadi ya pekee unayoweza kujipa, kumpa mfadhili wako.

Mwelekeo huu ndio utakupa sababu aidha kufanya mashauriano panapofaa ili uboreshe nafasi yako ya kufanikiwa.

Shirikiana na wenzio ifaavyo. Ukweli kwamba kinga na kinga ndipo moto huwaka una mashiko zaidi wakati huu unapoelekea kuikamilisha kozi yako katika ngazi hii. Kwa hiari yako mwenyewe jaribu kushauriana na wanafunzi wenzio. Tafuta msaada wao kila unapouhitaji huku nawe ukitoa wako panapofaa. Ni wengi wamefaana hivi na kusimuliana baadaye namna ushirikiano wao ulivyowafaa.

Usisahau kusema na mwalimu wako wa kila somo mara kwa mara kupata maelekezo yake na vidokezi vitakavyokufaa katika mtihani wako. Wahitaji hakikisho kutoka kwenye mtu aliye na mamlaka, na mwalimu wako anayo mamlaka katika somo lake, sema naye bila kuchoka.

Mwisho, kumbatia mtazamo chanya. Jihakikishie ufanisi. Iwe umeridhishwa na maandalizi yako hujaridhishwa, jihakikishie utafuzu. Woga hautabadili kitu ila kukusababisha kupoteza alama mbili tatu muhimu unazoziwania. Kwa hivi, ufukuzilie woga mbali! Mungu na akujalie afya na nguvu unapokaribia mwisho wa mbio yako ya maili kadha.

You can share this post!

KINA CHA FIKRA: Kujiamini kama kiambata cha ufanisi maishani

SAUTI YA MKEREKETWA: Ada inayotozwa na KICD ili kuidhinisha...