NASAHA: Tujipinde zaidi kwa uchaji Mungu katika Mwezi huu wa Ramadhani

NASAHA: Tujipinde zaidi kwa uchaji Mungu katika Mwezi huu wa Ramadhani

Na ATHMAN FARSI

Leo naomba tuangazie hili swala la amali bora zaidi katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Mijadala itakuwepo kuwa ni ibada hii ama ile ambayo ni muhimu ama bora zaidi lakini kwa mujibu wa Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.a) alipokhitimisha khotuba yake ya Ijumaa ya mwisho ya mwezi wa Shaaban, Ali bin Abitalib (a.s)anatuambia; “Baada ya kumaliza Mtume (s.a.w) hotuba hiyo, “nikasimama na nikamuuliza, ‘Ya Rasuu-lallaah, Amali gani bora kabisa katika mwezi huu mtukufu?’ Akajibu, ‘Uchaji wa Mwenyezi Mungu kwa kila kilichoharamishwa na kukatazwa’”.

Uchaji Mungu ni neno dogo sana na fupi mno lakini maana na upeo wake ni mkubwa zaidi na ni ngumu kivitendo sio rahisi. Kusali sunna, kusoma Qur’ani, kulisha masikini, kuvisha na mambo mengi yote ya kheri hayawezi kuwa sawa kabisa na Uchaji Mungu kwa sababu yote hayo ni sehemu moja tu ya uchaji Mungu.

Lakini kujitenga na madhambi na alichoharamisha Mwenyezi Mungu ni jambo la wajibu, si mwezi wa Ramadhani tu bali ni katika maisha ya mtu yote.

Kumcha Mungu ni jambo kubwa ambalo ibada nyingi za faradhi na za suna huchangia hili kapu kubwa la kumcha Mungu. Kumcha Mungu huandamana na subira. Huwezi kudai kumcha Mungu na na hauna subira. Kwa mfano muuni amefunga na majira ya saa kama kumi na moja jioni. Mtu akaja kumkejeli na kumtusi tusi kubwa tu.

Ikiwa huyu muumini hana subira basi itabidi audhike na kumjibu kwa matusi na hata kumchapa mwenye kumtusi. Ikiwa unamcha Mungu kisawa sawa, tukio hili litakupelekea kumkumbuka Mola wako mara moja na utampuuza huyu mtu na uendelee na hamsini zako.

Hebu tuangalie baadhi ya sifa za kumcha Mungu. Anayemcha Mungu anaamini mambo ya siri ya Allah (s.w.t) yaani mambo ya ghaib, anasimamisha swala kwa wakati wake, anatoa kwajili ya Mola wake, anaamini aliyoteremsha Allah (s.w.t), kuwa na yakini na siku ya akhera, anastahamili na kusibiri nyakati za raha na shida, mwenye kutimiza ahadi, mwenye kuomba msamaha kwa Mola wake kila wakati na kadhalika. Kwa hivyo, mwenye kuacha kila alichoharamisha na kufuata aliyoamrisha kwa yakini, mtu huyu atakuwa amefanya amali bora kuliko yote na huku ndiko kumcha Mungu.

Basi huyu muumini atapata bahati nzuri sana na atapata ujira bora zaidi kwa kuheshimu ugeni wake katika Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani.

You can share this post!

Mwanachuo akana kuua familia yake

Msako wa baharini wapunguza samaki