Habari Mseto

NASAHA YA RAMADHANI: Tuombe Mola wetu atusamehe na atusaidie tusirudie makosa yetu

April 3rd, 2024 2 min read

NA ALI HASSAN

ASSALLAM Aleykum ndugu yangu muumin wa dini hii tukufu ya Kiislamu. Tumejaaliwa leo hii kukutana tena kwa uwezo wake Allah (SWT) kukumbushana maneno ya kheri na kukatazana mawi kwenye mfungo huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Sasa hivi tukiwa kwenye fungu hili la kumi la mwisho wa Ramadhan, ni wakati mwafaka wa sisi waja kuulizana swali muhimu sana: Je, Mola wetu mwingi wa msamaha na rehema, ametusamehe madhambi yetu kwenye mwezi huu wa toba?

Hili swali linafaa liwe linamliza kila mmoja wetu huku mwezi huu wa msamaha ukitupungia mkono wa buriani. Na ili kukudhihirishia umuhimu wa mwezi huu kuwa mwezi wa toba, mwezi wa msamaha, ni kuwa Mola wetu ametenga kumi maalum la mwezi huu kuwa kumi la msamaha.

Allah (SWT) alijua kuwa sisi waja wake ni wakosaji, wasahaulifu, ndiposa akatuwekea nafasi, na satua maalum ya kuomba msamaha. Alijua kuwa hakuna mja mkamilifu, hapana mja asiyefanya makosa.

Hata hivyo, haifai mimi na wewe kuuchezaea msamaha huu, au nafasi hii ya msamaha tuliopewa.

Tunachomaanisha hapa ni kuwa iwe toba ya kweli, toba ya kihakika. Yaani unaomba radhi na unajiepusha na kuyarudia makosa ulioyafanya. Hata na wewe ndugu yangu hapo ulipo, akifanya mtu akaomba msamaha, utamsamehe. Lakini akiwa mara kwa mara anafanya kosa lile lile na kuomba radhi, utauona huo kama utani.

Vivyo hivyo, katika kuomba kwetu msamaha, kunatakiwa kuwa kuomba msamaha kwa kisawasawa, hasa kwenye mwezi huu wa msamaha. Na hapo kuwa na matumaini makubwa kuwa machozi yetu, kilio chetu, kimemfikia Allah (SWT) na tuna imani kuwa atatusamehe kutokana na wingi wa msamaha alionao Mola wetu Mtukuka.

Hadi mwezi huu wa toba unapofikia kikomo chake, ni yetu matumaini kuwa tutatoka katika darasa hili tukiwa weupe pe! Tukiwa tumezaliwa upya! Ya Allah (SWT) utusamehe madhambi yetu kwenye mwezi huu wa Ramadhan, na hata baada ya mwezi huu, na utupe nguvu na idili ya kutorudia madhambi. In Shaa Allah iwe kheri na wingi wa msamaha.

Saum maqbul