NASAHA ZA RAMADHAN: Mwenyezi Mungu hurehemu na kusamehe siku zote, tusikate tamaa

NASAHA ZA RAMADHAN: Mwenyezi Mungu hurehemu na kusamehe siku zote, tusikate tamaa

Na SHEIKH MOHAMED KHALIFA

TUKIWA tunaendelea kujibu maswali ya wasomaji wetu, leo nitalishughulikia swali la Ismail Omar wa Nakuru.

Yeye anauliza hivi, “Wakati tulipokuwa na kafyu ya saa mbili za usiku, nilikuwa nikimaliza kufungua mwadhini jioni najifungia nyumbani. Mara nyingi nilikuwa nikisinzia na kulala mapema. Ninahofia kuwa sijapata fursa ya kurehemewa katika Kumi la Kwanza na kusamehewa katika Kumi la Pili. Je, ipo nafasi ya kupata hayo yote katika kumi hili la mwisho?”

Ningependa kumwambia ndugu Ismail na wasomaji wengine wote kwamba Mtume Muhamad (SAW) asema, “Yule atakayesimama usiku wa Laylatul Qadir, atasamehewa dhambi zake zote.”

Tunavyojua ni kwamba usiku huo wa Laylatul Qadir ubora wake ni sawa na miezi elfu moja, au miaka 83. Usiku hizi kumi za mwisho tunazotarajia kuzikamilisha kesho au kesho kutwa, kutegemea na kuonekana kwa mwezi.

Mwenyezi Mungu (SWT) anasema kwenye Korani kuwa walioamini wapewe habari njema (Suratul Baqara aya ya 223). Habari hiyo njema anaifafanua kwa kusema, “Sema: Enyi waja wangu waliojidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.” (Suratul Zumar, aya ya 53). Hata kama Ramadhani imetoka, Mwenyezi Mungu husamehe wakati wowote. Mwenyezi Mungu (SWT) ni Ar-Rahman (Mwingi wa rehema).

Anaendelea kuwasamehe na kuwarehemu waja wake siku zote, maadamu umemwendea kwa unyenyekevu kutaka msamaha. Kwa hivyo, kusamehewa na kurehemewa havikuwekwa kwenye kumi la kwanza na la pili peke yake.

Lengo la kusema kumi la kwanza ni la rehema na la pili ni la maghufira, ni kuwafanya wanaofunga Ramadhani watafute fadhila hizo kwa wingi. Haina maana kuwa fadhila na rehema za Mwenyezi Mungu (SWT) hukoma kwenye hayo makumi mawili ya kwanza.

Namshauri ndugu Ismail na wale wote ambao wamekosa nafasi ya kufnya ibada kwa wingi kwenye makumi hayo, wasikate tamaa. Wajibidiishe kukesha usiku wakiomba rehema na msamaha. Pia wakumbuke Ramadhani yote milango ya pepo hufunguliwa na ya moto hufungwa. Milango ya kupokea msamaha na rehema ingali wazi.

You can share this post!

JAMVI: Mvutano ODM wazidisha ubutu kwa makali ya Raila

JAMVI: Ukimya uliogubika OKA ni ishara mbovu, Uhuru...