NASAHA ZA RAMADHAN: Sasa ni wakati bora wa kuzidisha kuisoma Qur’an

NASAHA ZA RAMADHAN: Sasa ni wakati bora wa kuzidisha kuisoma Qur’an

Na KHAMIS MOHAMED

KWA mipango ya Mwenyezi Mungu (SWT), tumeingia katika kumi la pili la mwezi ambao kawaida huwa wa kuzidisha kuisoma Qur’ani.

Ni katika mwezi wa Ramadhani ambapo Qur’ani iliteremshwa kwa Mtume (S.A.W), inatakiwa kwa Muislam kufanya bidii kuisoma angalau juzuu moja kwa siku ili aweze kumaliza msahafu ifikapo mwisho wa mwezi huu wa Ramadhan

Kusoma Qur’an katika mwezi wa Ramadhan kuna fadhila kubwa sana, kwanza ni kuadhimisha kushushwa kwake.

Pili, ni kuifuata sunnah ya mtume (S.A.W) na rafiki yake malaika Jibril walivyokuwa wakifanya kila usiku wa Ramadhani.

Na la tatu ambalo ni kubwa zaidi Mtume (S.A.W) Anasema ‘someni Qur’an kwani itakuwa shifaa’a (muombezi) siku ya Qiyama.

Na katika hadithi nyingine Anasema bwana Mtume (S.A.W) “Swaum na Qur’an vitamuombea mtu siku ya Qiyama.

Swaum itasema, Mola wangu nilimzuia kula na kunywa, sasa leo niache nimuombee shifaa’a. Na Qur’an nayo itasema nilimzuia kulala, Mola wangu, sasa leo niache nimuombee shifaa’a.

Na Allah (S.W) Atairuhusu funga na Qur’an iweze kuwa muombezi kwa mja huyo” (Sahih Muslim)

Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa Qur’an, na ndiyo mwezi ulioteremshwa Qur’an, kwa hivyo inafaa kuzidisha kusoma Qur’an ndani ya mwezi huu. Anasema mwenyezi Mungu (SWT), “Mwezi wa Ramadhani ambao umeteremshwa humo Qur’ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi.” (Al-Baqarah: Aya 185).

Ndungu Muislamu jipangie wakati uweze kuhitimisha Qur’an japo mara moja kwani Ramadhaan ndio mwezi ulioteremshwa Qur’an na hii ni Sunnah aliyokuwa akifanya Malaika Jibril kwa Mtume (S.A.W) kusoma naye Qur’an yote.

Kutoka kwa Ibn Abbas (R.A), “Mtume (SAW) alikuwa ni mbora (mwenye matendo mema) wa watu, lakini alikuwa mbora zaidi katika Ramadhan kwa sababu Jibril alikuwa akimjia kila usiku wa Ramadhan akimfundisha Qur’an.” [Al-Bukhaari].

Mwenyezi Mungu atukubalie funga zetu.

You can share this post!

KEMSA: Murathe apanga kujitetea mbele ya kamati

Wanafunzi 3 wa chuo kikuu waliotekwa nyara wauawa