Makala

NASAHA ZA RAMADHAN: Uislamu unaruhusu mume na mke kustarehe usiku wa Ramadhani

May 25th, 2019 2 min read

Na SHEIKH MOHAMED KHALIFA

KWA jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu.

Tunakutana tena baada ya mwaka mzima na leo kwa uwezo wa Allah (S.W.T) nitaangazia mada ambayo inatokana na swali la ndugu AbdulAziz Mwatambo kutoka Mwatate, kaunti ya Taita Taveta.

Yeye anataka kujua, Je, mtu anaweza kukutana kimwili na mkewe au mumewe baada ya saum?

Kufunga kwenyewe ni kujizuia kula, kunywa, kujitoa manii kwa mkono, kuingilia mwanamke wa halali au wa haramu.

Lakini katika kushiriki kimwili, hilo, ni kosa kubwa, haramu ambalo adhabu yake ni kubwa.

Yeyote anayekiuka amri ya kukataza kuingiliana kimwili na hata mkewe wakati wa mchana, kwanza atatakiwa yeye na mkewe wafunge kwa siku 60 mfululizo bila kupumzika.

Ikiwa hilo hawawezi, basi sheria inasema wawalishe masikini sitini.

Iwapo hayo yote hawayawezi, sheria inasema waachilie huru watumwa.

Hili la kumwachilia huru mtumwa haliwezekani sasa hivi, kwa kuwa enzi za watu kuwekwa watumwa zimepita.

Agizo kutoka kwa Mwenyezi Mungu

Mwislamu anatakiwa azingatie kuwa agizo la kumkataza kushiriki tendo la ndoa mchana wa mwezi wa Ramadhani linatoka kwa Mwenyezi Mungu, na ni dalili kuu ya kudhihirisha kuwa kweli mtu amejitolea kujinyima vyote vya halali kwa ajili ya kufuata amri ya Mola wake.

Kama ambavyo Baba wa Mataifa, Mtume Ibrahim (A.S) alitii amri ya Mwenyezi Mungu ambayo aliiona katika ndoto tu, sisi ambao tumepewa amri kwa maandiko hatuna sababu ya kuzikaidi.

Mtume Ibrahim baada ya kuwa ametengana na mwanawe kwa miaka mingi, alijitokeza tu siku moja na kumwambia Ismail kuwa ameona kwenye ndoto anamchinja. Ndoto ya mtume ilikuwa na ujumbe maalum

Alipomfahamisha hili, kijana Ismail alikubali bila maswali na akamwambia babake afanye lile aliloamriwa na Mola.

Walipokuwa wanajiandaa kutimiza amri hiyo, Mwenyezi Mungu aliona ukamilifu wa imani ya mtu na mwanawe. Badala yake aliwatumia kondoo ambaye walimchinja.

Kwetu sisi, Mwenyezi Mungu pia alifahamu dhiki anazopitia mtu na mkewe mchana wa Ramadhani, ambapo wanajizuia na kuepuka kuonana kimwili. Kwa sababu hiyo, amefanya usiku wa Ramadhani kuwa fursa ya mtu na mkewe kuonana kimwili. Lakini ifahamike kuwa sheria ni mtu na mkewe.

Mume na mkewe wameruhusiwa hadi atakapokaribia mwadhini wa swal ya Alfajiri na ni vyema waoge haraka na kuiwahi swala.