Michezo

Naser apigwa marufuku kwa kuvunja sheria za pufya

June 12th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa dunia wa mbio za mita 400 kwa upande wa wanawake, Salwa Eid Naser amepigwa marufuku ya muda kushiriki mashindano yoyote ya riadha baada ya kukosa kujiwasilisha kwa minajili ya kufanyiwa vipimo vya afya kubaini iwapo aliwahi kutumia pufya au la.

Mtimkaji huyo wa Bahrain mwenye umri wa miaka 22 alisajili muda wa sekunde 48.14 na kujizolea medali ya dhahabu jijini Doha, Qatar wakati wa Riadha za Dunia mnamo 2019. Muda huo ndio wa tatu wa kasi ya juu zaidi kuwahi kusajiliwa katika historia ya mbio za mita 400 kwa upande wa wanawake.

Naser ambaye ni mzawa wa Nigeria, alihamia Bahrain baada ya kupata uraia wa taifa hilo mnamo 2014. Ni mwanamke wa kwanza raia wa nchi ya bara Asia kuwahi kutwaa nishani ya dhahabu katika fani ya mbio hizo za mzunguko mmoja.

Kosa la Naser linamweka katika hatari ya kupigwa marufuku ya hadi miaka miwili kutoka kwa Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF).