Habari MsetoSiasa

Nashangazwa na Ruto kusalia kimya wandani wake wakizimwa – Echesa

June 4th, 2020 1 min read

NA IBRAHIM ORUKO

SHOKA la chama tawala cha Jubilee bungeni limezua hisia kali katika wandani wa Naibu Rais William Ruto eneo la Magharibi mwa nchi.

Wengi wa wandani wake wamekuwa wakishangazwa na hatua ya Dkt Ruto kusalia kimya huku wanasiasa wanaomuunga mkono wakivuliwa mamlaka na nyadhifa kuu bungeni.

Waziri wa zamani wa Michezo Bw Rashid Echesa ametapika nyongo hivi majuzi na kumsuta Naibu Rais kwa kimya chake baada ya mbunge wa Mumias Mashariki Benjamin Washiali kung’olewa kwa wadhifa wa kiranja wa walio wengi.

“Nina hakika kuwa Ruto angemsihi Rais Kenyatta kuhusu suala hilo, basi Bw Washiali hangetolewa kwa mamlaka hayo,” Bw Echesa akasema.

“Kumekuwa na habari kuwa Bw Atwoli na Bw Oparanya ndio wanaoongoza mabadiliko hayo, lakini sijawahi kuwaona Ikulu. Niliyemwona ni Naibu Rais, na kinachoshangaza ni kuwa hakusema neno kuhusu hatima ya Bw Washiali,” akaongeza.

Wabuunge 16 wanaoegemea upande wa Dkt Ruto tayari wamepewa barua za kuwaondoa kutoka kwa nyadhifa mbalimbali za kamati za bunge.