Makala

NASIKIA SAUTI YA MAMA: Tawasifu yenye mshabaha na maisha ya Ken Walibora

July 11th, 2018 2 min read

NA ENOCK NYARIKI

Jina la utungo: Nasikia Sauti ya Mama

Mwandishi: Ken Walibora

Kitabu: Riwaya

Mhakiki: Nyariki Nyariki

Mchapishaji: Longhorn

Kurasa: 158

Chembechembe za tawasifu ya Ken Walibora zinajitokeza katika riwaya yake ya kwanza kabisa ya Siku Njema (Ingawa mwenyewe Walibora aliahidi kwamba angekuja kuandika tawasifu yake.)

Kupitia kwa mhusika mkuu wa Siku Njema ambaye ni Kongowea Mswahili Walibora anampalia sifa sufufu mama yake. Usawiri wa aina hii wa mama unajitokeza katika Nasikia Sauti ya Mama ambapo Walibora anautambua Msaada aali wa mama yake si tu katika maisha yake ya udogo bali pia katika masomo yake.

Katika Siku Njema Komgowea Mswahili amesawiriwa kama msanii hodari katika uchoraji; jambo ambalo lilipaliliwa na mama mzazi katika elimu yake ya kwanza kabla ya elimu ya shule. Sanaa hiyo ya uchoraji inajitokeza tena katika tawasifu ya Nasikia Sauti ya Mama.

Chembe chembe za tawasifu hii zinajitokeza katika kazi nyingine kama vile Ndoto ya Almasi,Kufa Kuzikana na Kidagaa Kimemwozea ambapo Walibora ametaja miji mbalimbali na maeneo ya nyumbani kwao pamoja na wahusika kadhaa.

Miongoni mwa maeneo yanayojitokeza katika kazi hizo ni Sangura, Baraki, Cherengani miongoni mwa mengine.

Alhasili, yapo mengi ambayo Profesa Walibora ameyataja tu katika kazi zake za awali ambayo hatimaye yanajitokeza wazi katika Nasikia Sauti ya Mama.

Nasikia Sauti ya Mama ni kazi kuntu inayoyaelezea maisha ya utotoni ya Ken Walibora. Kupitia kwayo tunamwona Walibora akijitahidi masomoni kutoka kushika kilelecha cha mkia darasani,kugonea darasani kutofahamu lolote katika masomo hadi kuwa miongoni mwa wanafunzi bora zaidi masomoni.

Kichocheo chake kikuu katika kufikia ufanisi huu Ken Walibora anakiri ni mama yake. Watu wengine waliochangia ufanisi wa Ken Walibora katika utangazaji wa habari, utambaji wa hadithi na uandishi ni pamoja na babu wa kuukeni, Makali, bibi wa kuumeni, Sara Kusimba, baba yake, Bwana Murefu miogoni mwa wengine.

Vipo vipawa vingine vya Ken Walibora ambavyo vinajitokeza katika kazi hii ya Nasikia Sauti ya Mama. Ken Walibora alikuwa ashiki na mchezaji wa kabumbu , mwanariadha na mchoraji

Alhasili, Nasikia Sauti ya Mama ni tawasifu ambayo imefanikiwa kuyachora maisha ya utotoni ya Ken Walibora ambayo yalikumbwa na changamoto nyinyi zikiwamo maradhi,husuda za baadhi ya watu wa ukoo,umasikini miongoni mwa nyingine.

Mojawapo ya mbinu ambazo mwandishi amezitumia kwa ufanifu mkubwa katika kazi yake ni chuku na taswira.