Habari za Kaunti

Nassir afanya mabadiliko serikali ya kaunti kuboresha huduma

June 8th, 2024 1 min read

NA JURGEN NAMBEKA

GAVANA wa Mombasa Abdulswamad Nassir, amefanya mabadiliko katika uongozi wa kaunti hiyo akieleza kuwa mabadiliko hayo yalilenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wakazi wa Mombasa.

Mojawapo ya mabadiliko ya Gavana Nassir ni kuhusu usimamizi wa fuo za Mombasa ambazo kwa sasa zitakuwa chini ya Idara ya Maji, Mabadiliko ya Tabianchi na Maliasili. Idara hiyo pia itasimamia bustani na kushughulikia masuala ya usimamizi wa mazingira.

“Kwa kuhamisha usimamizi wa mazingira hadi kwa Idara ya Maji, Mabadiliko ya Tabianchi na Maliasili, tunalenga kusimamia mazingira kikamilifu,” akasema Bw Nassir katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Gavana Nassir alieleza kuwa idara ya kazi za umma pia ingesimamiwa na idara ya uchukuzi na miundomsingi, ili kuwezesha masuala ya maendeleo ya kimuundomsingi yameshughulikiwa kwa ujumla.