Habari za Kaunti

Nassir amkabidhi kiongozi wa Dawoodi Bohra ufunguo wa jiji

May 25th, 2024 1 min read

NA WACHIRA MWANGI

GAVANA wa Kaunti ya Mombasa Abdulswamad Sheriff Nassir amemkabidhi kiongozi wa kiroho wa jamii ya Dawoodi Bohra, Dkt Syedna Mufaddal Saifuddin, ufunguo wa jiji la Mombasa kama ishara ya kumkaribisha daima.

Heshima hiyo ilitolewa katika hafla ya kibinafsi nyumbani kwa Syedna Saifuddin jijini Mombasa.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Gavana Nassir, wafanyakazi wake, maafisa wa utawala wa kaunti, na ujumbe kutoka jamii ya Dawoodi Bohra.

Gavana Nassir akizungumzia umuhimu wa tukio hilo, alibainisha kuwa Dkt Saifuddin alikuwa mpokeaji wa kwanza wa ufunguo wa jiji chini ya uongozi wake.

Gavana alimpongeza kwa michango yake, hasa ule mradi wa kuvuna maji ya mvua uliozinduliwa wakati wa ziara yake iliyopita, ambao tayari umeanza kuzaa matunda.

“Tumefurahi sana na tunamshukuru sana Gavana kwa kutambua kujitolea kwa Syedna kwa sababu za kijamii na kumkabidhi heshima hii. Ni ushahidi wa urafiki na mshikamano wa muda mrefu kati ya uongozi wa jamii yetu na utawala wa kaunti,” mwakilishi wa jamii ya Dawoodi Bohra Bw Hamza Shuri akasema.

Zaidi ya wanachama 10,000 wa jamii ya Dawoodi Bohra wamekusanyika Mombasa kuhudhuria mahubiri na kupokea baraka kutoka kwa kiongozi wao wa kiroho.

Dkt Saifuddin ameshirikiana na wanajamii kutoa mwongozo na ushauri kuhusu masuala mbalimbali.

Mradi wa kuvuna maji ya mvua, uliozinduliwa mwaka 2023 kwa ushirikiano na Serikali ya Kaunti ya Mombasa, umekuwa na mafanikio makubwa.

Mradi huo umechochea miradi mingine sawa duniani kote, ikilenga kushughulikia ukosefu wa maji na kukuza usimamizi endelevu wa maji.