Nassir amrushia Shahbal fataki kali

Nassir amrushia Shahbal fataki kali

Na WINNIE ATIENO

Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir amewataka viongozi wengine kutoingilia siasa za uchaguzi wa ugavana wa Mombasa na kumuacha amenyane na mpinzani wake mkuu, mfanyabiashara Suleiman Shahbal.

Bw Nassir alisema kuna watu wanaomsaidia Bw Shahbal na wanafaa kuacha wakabiliane kwenye mchujo wa chama cha ODM.“Ninamwambia na ninamuomba hata rafiki yangu Ali Hassan Joho hizi siasa usiingilie.

Bado tuna imani na wewe. Licha ya kuwa katika uongozi wako ndio watu walipata kandarasi ya mabilioni, sasa fedha zinawawasha wanaona watanunua watu wa Mombasa,” alisema Bw Nassir.Bw Joho amewataka wakazi wa Mombasa kuamua wanayetaka kuwa gavana wao akisema hataingilia urithi wake.

Bw Nassir alisema amesimama kidete na chama cha ODM akimsuta Shahbal anayedai amekuwa akirandaranda kutoka vyama vya Jubilee, Wiper na sasa ODM. “Tulipigwa na vitoa machozi tukimtetea Bw Raila Odinga, tulifukuzwa na polisi, bungeni tumesimama kidete lakini wengine walikuwa wakichukua leseni za kandarasi,” alisisitiza.

Alimtaka Bw Shahbal kukomesha siasa za kejeli na masimango akisema siasa si vita ni kuuza sera.Wakati huo huo, baadhi ya wanasiasa wa vyama vya ODM na Jubilee wamewataka wakazi wa Pwani kuchukua kadi za kura ili kumpigia kura Bw Raila Odinga anayewania Urais.

Wabunge hao wanaompigia debe Bw Odinga walisema watajitolea mhanga kuhakikisha mgombea wao anamrithi Rais Uhuru Kenyatta kwenye uchaguzi mkuu Mwaka wa 2022. Vile vile waliwataka wakazi wa Mombasa kumuunga mkono Bw Nassir ambaye anawania kumrithi Gavana Hassan Joho.

Wakiongozwa na Kanini Kega (Kieni), Mohamed Hire (Lagdera), Teddy Mwambire (Ganze), Raphael Wanjala (Budalangi), Badi Twalib (Jomvu), Mishi Mboko (Likoni) na Esther Passaris (mwakilishi wa wanawake jiji la Nairobi) waliapa kumpigia debe Bw Odinga ashinde uchaguzi huo.

“Wapwani wamekuwa wakimuunga mkono Bw Odinga kwa miaka na mikaka, msikufe moyo tumefika hatima ya safari. Ni wajibu wenu kuchukua kadi za kura ili tupige kura kwa wingi. Kama Mlima Kenya sisi tumeamua Rais ni Odinga, lazima tusimame upande wa ushindi.

Gavana wa Mombasa ni Bw Nassir sababu amekuwa mstari wa mbele akitetea pwani,” alisema Bw Kega.Wabunge hao walimsuta Naibu wa Rais William Ruto kwa kuwahadaa Wakenya kwa kuwapa ahadi za uongo.

Wakiongea walipoweka jiwe la ujenzi wa shule ya upili ya wasichana ya Mekatilili wa Menza eneo la Ziwani wabunge walimpa changamoto Bw Ruto awaelezee Wakenya alichofanya akiwa mamlakani.

You can share this post!

Ukosefu wa usalama umezima maendeleo, wakazi walalamika

Shujaa yasuasua Safari Sevens ikipamba moto

T L