Nassir na Omar walenga wawaniaji wenza wa kike

Nassir na Omar walenga wawaniaji wenza wa kike

NA WINNIE ATIENO

MBUNGE wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, na aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar, wanatarajiwa kuteua wanawake kuwa wagombea wenza wao katika uchaguzi ujao wa ugavana Mombasa.

Idadi kubwa ya wanasiasa wanaowania ugavana Pwani wameonekana kujaribu kusawazisha vikosi vyao kwa msingi wa kijinsia, dini na kabila ili kuvutia kura nyingi iwezekanavyo.

Ijapokuwa Bw Nassir wa chama cha ODM hajatangaza wazi ni nani atakayekuwa mgombea mwenza wake, imebainika amepanga kumtangaza wiki hii na atakuwa ni mwanamke.

Kwa upande wake, Bw Omar wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), alithibitisha kuwa atamteua mwanamke kuwa mgombea mwenza wake lakini akataka wafuasi wawe na subira.

Naye aliyekuwa gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko (Wiper) alikuwa amemtangaza Mbunge wa Kisauni, Bw Ali Mbogo, kuwa mgombea mwenza wake katika kinyang’anyiro hicho cha kuwania urithi wa kiti cha Gavana Hassan Joho.

Katika kaunti ya Kilifi, Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, alimteua aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Jumuiya ya Kaunti za Pwani, Bw Emmanuel Nzai kuwa mgombea mwenzake katika kura ya ugavana.

Bi Jumwa atamenyana na aliyekuwa waziri msaidizi wa ugatuzi, Bw Gideon Mungaro (ODM), na Bw George Kithi (PAA) kuwania urithi wa kiti cha Gavana Amason Kingi.

Ingawa wawili hao hawajaweka bayana wagombea wenza wao, Bw Mung’aro alidokeza huenda akachagua mwanamke huku kikundi cha wanawake wa ODM katika Kaunti ya Kilifi kikimtaka kuchukua mwelekeo huo.

Katika Kaunti ya Kwale, Naibu Gavana, Bi Fatuma Achani alimchagua Bw Josephat Chirema baada ya kupata radhi za Naibu wa Rais William Ruto na Gavana Salim Mvurya.

Bw Chirema amekuwa diwani wa wadi ya Samburu/Chengoni tangu mwaka wa 2013.

Bi Achani, ambaye amekuwa naibu gavana tangu 2013, atamenyana na Prof Hamadi Boga (ODM), Lung’anzi Mangale (PAA) na Chirau Mwakwere (Wiper).

Prof Boga amemchagua Bi Safina Kwekwe kuwa mgombea mwenzake, ingawa Bw Mwakwere na Bw Mangale hawajawatangaza wagombea wenza wao.

Hata hivyo, Bw Mangale alisema atamchangua mwanamke.

Tana River, Hussein Dhado wa chama cha UDA amemchagua Bw Ibrahim Saney, aliyekuwa mwanachama wa bodi ya Mamlaka ya Ustawishaji wa Pwani. Awali alikuwa mbunge wa Garsen.

Hata hivyo, gavana wa sasa Bw Dhado Godana (ODM) hajachagua mgombea mwenza baada ya kukosana na naibu gavana Bw Salim Batuyu.

Lamu, Gavana Fahim Twaha wa chama cha Jubilee hajatangaza rasmi mgombea mwenza wake baada ya naibu wake kuhamia UDA akimpigia debe Naibu wa Rais.

Mpinzani wake wa karibu, aliyekuwa gavana Bw Issa Timamy wa ANC amemchagua Bw Raphael Munywa kuwa mgombea mwenza.

Wengine wanaogombania kiti hicho ni pamoja na aliyekuwa naibu gavana wa Bw Timamy, Bw Erick Mugo na Bi Umra Omar (Safina).

Huko Taita Taveta, Gavana Granton Samboja (Jubilee) anaendelea kupata ushindani mkubwa kutoka kwa aliyekuwa Gavana Bw John Mruttu wa UDA.

Wawili hao hawajatangaza wagombea wenza. Bi Patience Nyange anagombania kupitia chama cha Narc Kenya.

  • Tags

You can share this post!

Ndoto za nyota wa KCPE zafifia kwa kukosa karo

Mshindi wa EPL msimu huu huenda akapatikana katika wiki ya...

T L