Makala

Nassor Kharusi: Mazingira ya Zanzibar yalipalilia kipaji changu cha ushairi

October 11th, 2020 2 min read

Na HASSAN MUCHAI

NASSOR Hilal Kharusi ni nembo ya ushairi na mpenzi mahiri wa magazeti ya Taifa Leo na Taifa Jumapili.

Mzaliwa huyu wa visiwani Zanzibar alikulia katika mji huo unaosifika kama johari ya historia katika ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki.

Alianza kunoa makali yake katika shule ya msingi za Kajificheni kabla ya kujiunga na shule za upili za Vikokotoni,Shangani,Forodhani na Tumekuja.

Alikuwa na uraibu wa kipekee wa kusoma vitabu na magazeti akiwa angali bado na umri mdogo. Haswa, alilenga kurasa za mashairi. Kama ilivyo, alijaribu kuyaghani akiwa na mapumzikoni.

Baadaye alijifunza kuandika na kuhifadhi daftarini kazi zake hadi siku moja alipotokea rafiki yake na akashangazwa na ubunifu wake. Rafiki yake hakuamini kwamba, ni yeye aliyekuwa akiandaa kazi zile kutokana na umri wake mdogo. Alimpa mkono wa tahania na kumhimiza kutorudi nyuma.

Muda si muda, alifanikiwa kuandika kitabu chake cha kwanza, diwani ya Barsheba Safari. Alivutiwa na vitabu vya washairi wa kale kama vile Shaaban Robert, Muyaka bin Haji na Profesa Said Ahmed.

‘’Mshairi ambaye nilianza kumjua mapema alikuwa Bwana Abdilatif Abdalla kwa sababu nyumbani kilikuwapo kitabu cha Sauti ya Dhiki na baba yangu akanieleza yaliyompata mwandishi huyo.

Kwa jumla, mazingira ya wakati ule yaliathiri malezi yangu kwa sababu hayakuwa ya mtu mmoja bali ya wazazi nyumbani, majirani, walimu na jamii nzima kwa jumla,” alisema Khilal kwenye mahojiano.

Kwenye hafla za shule, alikuwa akipewa nafasi ya kusoma mashairi yaliyotungwa na walimu. Baadhi ya wanafunzi wenzake walipata msisimko na mvuto wa kufuata nyayo zake walipogundua ana kipaji hicho cha kipekee.

‘’Walimu wangu wa shule ya msingi marehemu Bi Keis Ali Saleh na Bi Fatma Qamus wana nafasi ya pekee kwenye nafsi yangu kwa namna walivyonifunza,lakini pia kunipa mkono wa tahania nilipofanya vyema.

‘’Babangu Bw Hilal Mohammed alinifanya kupenda kusoma kwani nikiwa mdogo, alizoea kuninunulia vitabu nami nikaanza kusoma na hapo ndipo nikapata raghba ya uandishi.’’ asema.

Washairi waliomchochea kwa utunzi wao ni pamoja na Haji Gora, Mohammed Ghassani na Profesa Said Ahmed. Asema kazi zao ni za kiwango cha juu.

Akiwa mdogo, alikuwa akishangazwa na falsafa ya baadhi ya mashairi kwenye nyimbo asili za Taarab na mashairi ya kurutubisha akili na kushibisha nafsi. Ubeti mmoja wa Shairi aliosikia utotoni unasema:

Binaadamu Wengineo wana siri,

Hawadumu Kwa sifa zilo nzuri,

Kama ndimu. Tamu mwishowe shubiri .

Ubeti huu ulimfanya awazie sana kuhusu ndimu na tabia yake na akaona urari baina ya hulka ya maumbile ya tunda hili na binadamu. Akaamua kila kilichopo duniani huwa na uhusiano na maisha ya binadamu.

Nassor Khilal ni mwandishi na ameandika vitabu vitatu ambavyo ni; diwani ya Barsheba, Safari, Hisia Zangu na Siku Zapishana.

Amewaahidi mashabiki wake kuwa hivi karibuni atachapisha kitabu ambacho ni mswada aliouwasilisha kwenye mashindano ya Mabati ambapo alikuwa mmoja wa washairi walioorodheshwa miongoni mwa washindi mwaka 2019 na shairi lake ‘Mama usihuzunike’.