Shangazi Akujibu

Natafuta mwanamke mwaminifu nimuoe, je, nitampata?

May 5th, 2024 1 min read

Kwako shangazi. Nina miaka 27. Ninatafuta mwanamke mwaminifu kwa uhusiano wa kimapenzi kisha nimuoe baadaye tuishi pamoja. Je, nitaweza kumpata?

Wapo wanawake wengi wanaotaka kuolewa. Lakini baadhi yao hawana sifa unazotaka. Kuwa na subira katika harakati zako za kutafuta hadi utakapompata anayekufaa.

Nimeshindwa kuacha penzi la mume wa wenyewe

Kwako shangazi. Mpenzi wangu ni mwanamume aliye na familia. Nina miaka 25. Nataka kumuacha nitafute mume lakini nimeshindwa. Kila akinipigia simu tu, hisia zake hunasa mawazo yangu tena. Nifanyeje?

Kwa nini unapoteza wakati wako kwa mume wa mwenyewe mwanamke mchanga kama wewe? Iwapo umeamua kumuacha, ni lazima uvunje uhusiano huo. Epuka kabisa kukutana na kuwasiliana naye.

Miaka mitano imepita tangu tuachane ila asema bado ananipenda

Mambo shangazi? Nilikatiza mawasiliano na mpenzi wangu baada ya kupoteza simu. Juzi tulikutana mjini baada ya miaka mitano akaniambia bado ananipenda. Nampenda pia lakini nina mwingine. Nifanye nini?

Maisha yako ya kesho yanategemea maamuzi yako ya leo. Kama bado unampenda huyo wa awali, mwelezee huyo mwingine ukweli ili muachane urudi kwa chaguo la moyo wako.

Ni mwaka wa nne nikitegea asali lakini bado sijapewa

Salamu shangazi. Huu ni mwaka wangu wa nne katika uhusiano wa kimapenzi. Mpenzi wangu amekataa kabisa kunifungulia mzinga ilhali anasisitiza ananipenda. Nafikiri ananihadaa. Nishauri.

Si lazima mpenzi wako akubali ombi lako ili kuthibitisha anakupenda. Hiyo itakuwa haki yako ukimuoa. Kama amekuhakikishia anakupenda, huna sababu ya kumshuku. Kuwa na subira.