Michezo

Nataka kufurahia soka ya Ufaransa, asema Griezmann

June 12th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MABINGWA wa La Liga nchini Uhispania Barcelona wamepata pigo jingine baada ya mshambulizi wa Atletico Madrid Antoine Griezmann kusema hana uhakika kwamba atashiriki mechi za ligi hiyo msimu wa 2019/20.

Barcelona wamekuwa katika mstari wa mbele kutwaa huduma za mshindi huyo wa Kombe la Dunia aliyechezea Atletico kwa muda wa miaka mitano.

Duru hata hivyo zinaarifu kwamba Griezmann huenda akajiunga na Mabingwa wa Ufaransa PSG baada ya klabu hiyo kutokuwa na hakika iwapo nyota Kylian Mbappe na Neymar watawasakatia msimu ujao.

Ingawa hivyo, Griezmann naye anaonekana kutulia na kuwa mwenye subira huku tetesi zikidi kushamiri kuhusu hatima yake msimu wa 2019/20.

“Kuna hitaji kubwa ya kutulia na kusubiri. Ningependelea hatima yangu ijulikane haraka iwezekanavyo kuliko mtu yeyote ila kuna haja kubwa ya wote kusubiri mwelekeo wa mambo,” akasema Griezmann baada ya mechi za kufuzu kwa Euro 2020 dhidi ya Andora mnamo Jumanne Juni 11.

“Sijui kama nitasalia Uhispania lakini nina hakika kwamba katika muda wa wiki mbili nitafahamu hatima yangu. Nitaka tu kushiriki soka na kujifurahisha,” akaongeza Griezzman, 28.

Mwanadimba huyo amekuwa nchini Uhispania tangu mwaka wa 2014 na alichezea Real Sociedad kabla ya kujiunga na Atletico Madrid.

Atletico ilimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Barcelona waliotwaa ubingwa wa La Liga huku Griezmann akifunga mabao kwenye ligi hiyo na mengine 15 kwenye mashindano mengine 21.