Habari MsetoSiasa

Natamani kuwa kama Raila, ana roho safi sana – Moses Kuria

July 24th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

Raila ni mtu wa maajabu na mwenye roho safi ajabu. Haya ni maneno ya mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, ambaye aidha alimsifia kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kuwa rafiki yake wa karibu sana, ambaye hawawezi kukosana.

Kulingana na Bw Kuria, Bw Odinga si mtu wa kinyongo ama kukaa na chuki rohoni mwake, akisema hajawahi kumwona kiongozi mzuri kiasi hicho.

Mbunge huyo alikuwa akimsifu Bw Odinga hivyo alipokuwa katika mahojiano na mwanahabari Tom Gachoka, katika runinga ya KTN News.

Aliendelea kueleza jinsi angependa kuwa kama Raila, kuonyesha mapenzi yake kwa kiongozi huyo.

“Raila ni mtu wa maajabu, hana chuki, nikikua mkubwa ningependa kuwa kama yeye. Tuna uhusiano spesheli na hakuna atakayeubadilisha,” akasema mbunge huyo.

Maneno yake siku hiyo yalikuwa kinyume na kawaida yake kwani amenukuliwa mara kadha mbele ya umma akitumia matamshi ya chuki kumlenga Bw Odinga, ikiwamo wakati mmoja aliposema kiongozi huyo anafaa kuuawa.

Bw Kuria hata amewahi kuzuiliwa seli kwa wiki moja kwa kutumia matamshi ya chuki dhidi ya kiongozi huyo, na hivyo maneno yake ya Jumatano yalikuja bila kutarajiwa.