Makala

NATASHA NJOKI: Filamu ya '12 Years A Slave' imenivutia sana

November 14th, 2020 2 min read

NA JOHN KIMWERE

ANAAMINI anacho kipaji cha kufanya vizuri katika tasnia ya uigizaji na kunasa tuzo za kimataifa kama Oscars na Grammys kati ya zingine. Anasema ingawa hajapata mwanya kuonyesha uwezo wake amepania kujituma mithili ya mchwa kuhakikisha anatimiza azma yake katika sekta ya wanamaigizo.

Pia anatamani kuibuka maarufu katika tansnia ya uigizaji angalau kutinga kiwango cha mwigizaji wa Hollywood mzawa wa hapa Kenya, Lupita Nyong’o.

Natasha Njoki Wambui maarufu Tasha_Nashaa anaorodheshwa kati ya wasanii wa kike wanaopania kuvumisha ulingo wa burudani ya maigizo hapa nchini. Kando na kushiriki majaribio kwenye juhudi za kusaka ajira ya maigizo binti huyu ni video vixen na mpodoaji (Makeup Artist).

”Nilianza kushiriki maigizo nikiwa mdogo kanisani ambapo kufikia sasa bado nina ndoto ya kuibuka mahiri duniani,” alisema na kuongeza kwamba anaamini muda utakapowadia hamna atakayezuia.

12 YEARS A SLAVE

Kando na kwamba alidhaamiria kuwa mwigizaji tangia akiwa mtoto anasema aliweza kuvutiwa zaidi na masuala ya sanaa ya maigizo alipotazama filamu za mwigizaji Lupita Nyong’o. ”Kiukweli nilipotazama filamu ya 12 Years a slave ilinivutia sana na kutamani kuzamania zaidi katika masuala ya maigizo.

Anasema hapa nchini angependa sana kufanya kazi na waigizaji kadhaa wanaofanya vyema akiwamo Gloria Songoro ambaye hushiriki kipindi cha Selina ambacho hupeperusha kupitia runinga ya Maisha Magic. Mwingine akiwa Sarah Hassan aliyekuwa akishiriki kipindi cha Tahidi High ambacho hupeperushwa kupitia Citizen TV.

FAMOUS IN LOVE

Kwa waigizaji wa Afrika anatamani kujikuta jukwaa moja na Lesley-ann Brandt mzawa wa Afrika Kusini ambaye ameshiriki filamu iitwayo ‘Lucifer.’ Kadhalika yupo msanii wa maigizo ya Kinigeria (Nollywood), Pepi Sonuga ambaye ameshiriki filamu kama ‘Famous in Love.’

CHANGAMOTO

Kama ilivyo kwa sekta zingine binti huyu aliyezaliwa mwaka 2000 anasema jukwaa la uigizaji nimefurika maafisi wengi tu ambao hupenda kushusha hadhi ya wanawake. ”Binafsi nimekutana na visanga kadhaa ambapo wanaume hunijia na kutaka tuwe na mahusiano ya kimapenzi ili kunisaidia kupata ajira katika kampuni zao,” akasema na kutoa wito kwa maprodusa wakomesha mitindo hiyo ili kukuza talanta za wasanii wanaokuja.

Msichana huyu anashauri wenzake kuwa makini kwa kile wanachohitaji wanapojiunga na sekta ya uigizaji. ”Kama ilivyo kwa sekta zingine jukwaa la maigizo kamwe mambo sio mteremko limejaa pandashuka nyingi ambapo ni rahisi kwa msanii kupoteza mwelekeo endapo atasahau azma yake,” akasema.

Kadhalika anashauri kuwa uigizaji unahitaji kuvumilia maana mafanikio hayapatikani rahisi. Anadokeza kuwa ingekuwa vizuri kama serikali inaweza kutega fedha za kusaidia sekta ya uigizaji maana wapo wasanii wengi tu humu nchini ambao hawajapata nafasi kuonyesha vipaji vyao.