Habari za Kaunti

Natembeya atisha kufuta madaktari na kuajiri wapya kutoka Uganda

April 24th, 2024 1 min read

NA EVANS JAOLA

GAVANA wa Trans Nzoia George Natembeya ametishia kuwafuta kazi madaktari wa kaunti hiyo wanaogoma na kuajiri wapya kutoka Uganda kuchukua nafasi zao.

Mkuu huyo wa kaunti alisema anapanga kuajiri madaktari kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki iwapo madaktari hawatasitisha mgomo wao ambao umelemaza huduma katika hospitali za umma kwa mwezi wa pili sasa.

“Kwa sababu kanuni za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaruhusu watu kuhamia nchi wanachama kufanya kazi, kuuza bidhaa na kutoa huduma, nitakachofanya ni kutangaza nafasi za kazi na kuajiri madaktari kutoka Uganda. Serikali ya kaunti ya Mandera imeajiri madaktari kutoka Ethiopia na wanafanya kazi,” Bw Natembeya alitisha.