Makala

Nathan Abuti: Anatumia baiskeli kueneza ujumbe wa amani

March 2nd, 2019 4 min read

Na SAMMY WAWERU

UNAPOMTAZAMA akiendesha baiskeli yake iliyopambwa kwa bendera za mataifa mbalimbali, utadhani anafanya hivyo kwa ajili ya kuonyesha umaridadi tu wa kawaida.

Kuanzia mbele hadi nyuma, ina zaidi ya bendera 10 ikiwamo ya Kenya, nchi zinazounda eneo la Maziwa Makuu, Amerika, Israeli, na Uingereza, hizo zikiwa chache tu kuzitaja.

Ina vijibango mbalimbali vyenye jumbe maalumu, na Bw Nathan Abuti anasema huitumia kuzuru maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuhubiri ‘amani, upendo na umoja wa taifa’.

“Kila mwaka wa uchaguzi mkuu, Kenya haikosi kushuhudia ghasia na machafuko. Taifa hili linahitaji kuunganishwa, tuzike katika kaburi la sahau ukabila tuwe kabila moja liitwalo Kenya na ndio maana ninaeneza ujumbe wa amani, upendo na umoja,” anasema Bw Abuti.

Shughuli hii na ambayo ni gange yake ya kila siku aliianza 2016, mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 2017 uliokumbwa na ghasia.

Rais Uhuru Kenyatta aliyewania kuhifadhi kiti chake kwa awamu ya pili na ya mwisho kwa tiketi ya Jubilee (JP) na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga wa Nasa, ndio walikuwa wagombeaji wakuu.

Ili kuangazia mizozo inayozuka, Bw Abuti ametembelea si mara moja ama mbili maeneo yanayotajwa kuwa tata wakati wa uchaguzi. Anasema maandamano yanayotokea na wahusika kuishia kufunga barabara, kuchoma biashara za watu, magari na nyumba, kila mmoja anafahamu wazi hayatatui migogoro ila huendelea kuongeza umaskini. “Vita huzidisha adui kama vile janga la njaa. Unapoteketeza biashara, nyumba, magari na kufunga barabara unatarajia mazao yatakuwa yapi iwapo si ufukara?” akahoji wakati wa mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Dijitali.

Anapenda kujiita ‘Mkenya Balozi wa amani’ na anasema ufisadi ni janga lingine linalosababishwa na wapiga kura wanaochagua viongozi wasioafikia vigezo vinavyohitajika, kwa kile anataja kama kuchochewa na ukabila na ubinafsi.

Anaongeza kueleza kwamba hali ngumu ya maisha inayoshuhudiwa inasababishwa na ufisadi kwa kuwa raslimali haziwafikii wananchi kule mashinani kwa sababu ya kufujwa na viongozi.

Bw Nathan Abuti maarufu Balozi wa Amani Kenya wakati wa mahojiano na Taifa Leo. Picha/ Sammy Waweru

Kwa hili, anasema ni kinaya kabisa na demokrasia inayodaiwa kuwepo nchini.

“Taifa linalothamini demokrasia, matukio kama hayo hayafai kuwepo. Uhuru ni kila raia kufikiwa na huduma za umma na kupata raslimali bila kufujwa kwa kuwa ndiye mlipa ushuru,” afafanua.

Hamasisho lake kuleta utulivu na amani kwa kutumia baiskeli, linaendelea wakati ambapo Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Bw Raila Odinga wanaendeleza kampeni ya utangamano wa kitaifa kupitia ziara zao maeneo mbalimbali nchini.

Hii ni baada ya viongozi hao mwaka 2018 kutangaza kuweka kando tofauti zao kisiasa, kwa shabaha ya kuunganisha taifa.

Kupitia salamu za maridhiano maarufu handshake Machi 9, 2018, Rais Kenyatta na Raila walibuni kamati maalumu ‘Building Bridges Initiative (BBI)’, yenye wanachama 14 ili kutegua kitendawili cha kiini cha migongano kila miaka ya chaguzi kuu.

Mbali na kuangazia suala la ukabila, BBI pia ilitwikwa jukumu la kutathmini janga la ufisadi, ugavi wa raslimali ya umma, miongoni mwa changamoto zingine zinazotishia utangamano wa taifa.

Kamati hiyo inaendelea kukusanya maoni ya wananchi kupitia vikao vya umma, na tangu ilipozinduliwa rasmi ilipewa kipindi cha mwaka mmoja kuandaa ripoti ya pamoja itakayowasilisha kwa Rais Kenyatta na Raila, ambaye 2018 alichaguliwa na Muungano wa AU kusimamia maendeleo ya muundo msingi Afrika.

Rais amenukuliwa na vyombo vya habari akisema “hili jambo la mshindi wa wadhifa wa urais kunyakua yote sharti lifikie kikomo”, kama njia mojawapo kutatua mizozo ya baada ya uchaguzi.

Ili kuafikia hayo yote, Abuti anasema sharti Wakenya waitikie kuwa kitu kimoja a kujiepusha na siasa duni, wapendane na wasaidiane kukuza nchi.

“Sitaacha kukumbusha viongozi kuwa wao ndio kilelezo chetu. Waunganishe Wakenya kwa kuhubiri siasa za amani kama tunavyoona Rais Kenyatta na Raila Odinga wakifanya,” aelezea.

Uungwaji mkono

Kauli yake inatiliwa mkazo na Bw Martin Mbogo, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

“Jukumu la utangamano wa taifa lisiachiwe Rais na kiongozi wa upinzani, liwe la viongozi wote na wananchi kwa jumla. La sivyo, tatizo la migawanyiko kwa msingi wa ukabila na kisiasa halitabainika, na machafuko ya baada ya uchaguzi yataendelea kutokea,” ashauri mdau huyu.

Wakati wa mahojiano Abuti alisema husafiri kwa baiskeli yake ya kipekee kutoka Nairobi hadi Kisumu, Uasin Gishu, Kakamega, Bungoma na Busia, ili ujumbe ufikie kila mmoja. Pia amezuru kaunti zisizo mbali na jiji la Nairobi kama Nakuru, Machakos, Nyeri, na Kirinyaga.

“Iwapo sina pesa za kukodi chumba cha kulala, giza linapobisha hodi hujisitiri kwenye veranda ya duka kupitia idhini ya mmiliki wake. Huvumilia kijibaridi kikali usiku, kwa kuwa huu ni wito wa uzalendo,” anasimulia.

Kando na changamoto hiyo, alisema jitihada zake kuhubiri amani zinaandamwa na ukosefu wa usalama akidokeza kwamba kuna baadhi ya wanaofikiria hupokea donge nono kutoka kwa serikali. Hii ni gange anayoifanya kila siku, na ni mume na baba wa mtoto mmoja, iweje basi Bw Abuti anamudu kukidhi mahitaji ya familia yake kikamilifu? Anajibu; “Aliyevalia kiatu ndiye hujua kinapombana, hupima nguvu zangu (akimaanisha uwezo) na zinapoishia ninakomea hapo. Ninategemea Mungu, yeye ndiye hunifungulia njia.”

Anasema hajawahi kupata ufadhili wowote kutoka kwa serikali, huku mipango ya kuongea ana kwa ana na Rais Kenyatta Ikulu ikigonga mwamba.

“Msaada niliopata 2017 ni wa Moses Kuria (mbunge wa Gatundu Kusini) wa Sh1,000,” anafichua.

Changamoto nyingine ni kudunishwa na baadhi ya wahudumu wa matatu na magari.

“Oktoba 16, 2018 eneo la Kiambaa kaunti ya Uasin Gishu nikirejea jijini Nairobi niligongwa na gari, nikapata majeraha na baiskeli ikaharibika. Niliokolewa na dereva wa lori, aliyenipa hela za kupata matibabu na kukarabati baiskeli,” asema, akihimiza wenye nia mbaya badala ya kufanya kitendo kama hicho washirikiane naye.

Abuti 75, ni mzaliwa wa Butere, Kakamega na anaishi katika kaunti ya Kiambu. Alistaafu mwaka wa 1994, ambapo alikuwa akihudumu katika shirika la Posta Kenya.

Anashikilia kwamba licha ya kula chumvi, atatia nanga juhudi zake kueneza ujumbe wa amani, upendo na utangamano, Kenya itakapozika tofauti za kikabila, na raia kukiri hili ni taifa moja, chini ya kabila moja la Mungu.