Nation FC yazima Dagoretti Hot Stars na kutwaa ubingwa wa Bosibori Cup

Nation FC yazima Dagoretti Hot Stars na kutwaa ubingwa wa Bosibori Cup

NA JOHN ASHIHUNDU

NATION FC ni miongoni mwa timu zilizotia fora Jumapili wakati wa fainali za kuwania ubingwa wa Norah Bosibori katika eneo la Dagoretti Kaskazini.

Kikosi hicho cha kampuni ya Nation Media Group kilitwaa kombe la Wadi ya Kilimani baada ya kuitandika Dagoretti Hot Stars kupitia mikwaju ya penalti.

Baada ya mechi hiyo kumalizika kwa sare ya 1-1, mwamuzi Juma Turke aliamuru mikwaju hiyo ipigwe ambapo Nation walishinda kwa mabao 6-5.

Sammy Mumicha alifunga bao katika muda wa kawaida wakati bao la Hot Stars lilimiminwa wavuni na Robert Mbugua.

Penalti za Nation zilifungwa na Tonny Omondi, Antony Ochieng’, Bennis Obe, Kevin Lwangu, Titus Mbithi na Michael Ndung’u.

Kikosi cha Nation FC katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Gatina, Dagoretti, Nairobi Januari 16, 2022. PICHA/ JOHN ASHIHUNDU

Waliofungia Hot Stars ni Godfrey Murungi, Robert Mbugua, Derrick Ouma, Joshua Kiodi na Brian Machisu huku William Olicho akipoteza baada ya mkwaju wake kuzuiliwa na kipa George Ipomai.

Katika fainali za Wadi nyingine matokeo yalikuwa: Jet FC 1 Boca Junior 0, Escalators 4 Hardy Bay 3, Dago Sisters 1 Joylave 0, Waruku Sporttif 4 UoN Virkings 2.

Zaidi ya timu 40 zilishiriki kutoka wadi zote tano za Dagoretti za Kilimani, Kawangware, Keleleshwa, Gatina na Kabiro zilishiriki.

Washindi na timu zilizomaliza katika nafasi ya pili walipata mavazi na pesa taslimu kutoka kwa mdhamini Norah Bosibori ambaye ni miongoni mwa watakaowania kiti cha ubunge cha Dagoretti Kaskazini.

Bosibori aliwashauri wachezaji umuhimu wa michezo kwa afya ya mwili na akili yao.

Norah Bosibori (wa nne kutoka kushoto, walioketi) pamoja na wageni waliohudhuria fainali ya Bosibori Cup. PICHA/ JOHN ASHIHUNDU

Aalitaka walezi, wazazi kuhakikisha watoto wao wanafanya mazoezi kila wanapokuwa na wakati wa kufanya hivyo.

“Nyote mnakubaliana nami kwamba mtu yeyote anayefanya mazoezi ni vigumu sana kupata maradhi ya mara kwa mr kwa sababu anafanya mazoezi,” aliongeza.

Alisema vijidudu vingi vya maradhi ushambulia mtu akiwa dhaifu katika mwili wake, lakini ni vigumu kushambulia mtu anayefanya mazoezi kwa sababu mazoezi anayofanya yanamweka katika hali nzuri kila wakati.

“Ukiwa mtu wa mazoezi muda wote unakuwa na furaha tu, ni wachache sana huwa hawana furaha lakini asilimia kubwa ya wanamichezo akili yao inakuwa imetulia hivyo kwao michezo ni furaha pia.

Aliwakumbusha vijana kwamba faida nyingine ni kuwa mchezaji anaajiriwa, huku akiwakumbusha kwamba baadhi ya wanamichezo duniani wanalipwa vizuri, na sasa michezo kwao ni ajira kubwa inayowalipa vizuri sana.

“Enyi mlio na vipaji ipo siku mtafurahia kwa wanamchezo kwani mtaona faida yake wakati huo utakapofika,” aliongeza Bosibori ambaye aliandamana na Kizito Makhuyi ambaye pia ametangaza kuwania kiti cha udiwani, Wodi ya Kabiro kwa tikiti ya ODM

  • Tags

You can share this post!

Serikali yamwaga maafisa 100 kukabili uhalifu Lamu

KEMSA yatangaza zabuni nyingine ya bidhaa za corona sakata...

T L