Nations League: Italia kualika Uingereza uwanjani San Siro mnamo Septemba 2022

Nations League: Italia kualika Uingereza uwanjani San Siro mnamo Septemba 2022

Na MASHIRIKA

MECHI ya Nations League itakayokutanisha Uingereza na Italia ugenini mnamo Septemba 23, 2022 itachezewa katika uwanja wa San Siro jijini Milan.

Itakuwa mara ya kwanza kwa Uingereza kusakatia mechi katika uwanja huo ambao umekuwa ukitumiwa na Inter na AC Milan kwa ajili ya mechi zao za nyumbani tangu 1939.

Mara ya mwisho walipokutana, Italia walizamisha chombo cha Uingereza kupitia penalti kwenye fainali ya Euro 2020 ugani Wembley. Hata hivyo, mashabiki wa Uingereza walizua vurugu na fujo wakati wa gozi hilo.

Mchuano wa mkondo wa kwanza wa Nations League utakaokutanisha Uingereza na Italia ugani Molineux mnamo Juni 11, 2022 hautahudhuriwa na mashabiki baada ya kikosi hicho cha kocha Gareth Southgate kuadhibiwa.

Uingereza watasafiri hadi Budapest kwa mchuano wao wa kwanza wa Kundi A3 dhidi ya Hungary mnamo Juni 4. Mechi hiyo itachezwa pia bila mashabiki kutokana na adhabu ambayo Hungary walipokezwa kutokana na fujo iliyozuliwa na mashabiki wao wakati wa fainali za Euro 2020.

Uingereza watamenyana na Ujerumani jijini Munich mnamo Juni 7, 2022 kabla ya kuwa wenyeji wa Italia na Hungary ugani Molineux mnamo Juni 11 na 14 mtawalia.

Baada ya kumenyana na Italia jijini Milan, Uingereza watafunga kampeni zao za makundi ya Nations League dhidi ya Ujerumani mnamo Septemba 26 uwanjani Wembley.

Baada ya mechi hizo, masogora hao wa Southgate wataelekeza macho yao kwa fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar kuanzia Novemba hadi Disemba 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

  • Tags

You can share this post!

Antonio Conte kuendelea kuwa kocha wa Tottenham msimu ujao

Kalonzo nje ya urais, sasa kurejea Azimio wiki ijayo

T L