Dondoo

Natoka na mumeo, kipusa ajigamba

April 23rd, 2019 1 min read

Na MIRRIAM MUTUNGA

SOUTH B, NAIROBI

SINEMA ya bure ilishuhudiwa kwenye ploti moja mtaani hapa vipusa wawili walipotwangana makonde mmoja alipomwambia mwenzake mumewe alikuwa mpenzi wake kwa muda mrefu.

Kulingana na mdokezi, kipusa huyo alikuwa akifanya kazi kwenye baa moja mtaani hapa na alikuwa na mazoea ya kulewa chopi. Fununu za mitaani zinatuarifu kwamba kipusa huyo alikuwa na tabia ya kuwateka wanaume.

Siku ya kisanga, alikuwa amelewa chakari na akaanza kupayukapayuka hadi akafichua siri.

“Mimi nimeumbwa nikaumbika na ndio maana nimemvutia mumeo hadi akaingia kwenye mtego wangu. Mumeo amekuwa mpenzi wangu kwa muda mrefu na bado mapenzi yetu yamepamba moto,” kipusa aliropoka alipokutana na mwenzake.

Kusikia hivyo mwenzake alichemka kwa hasira na kumfokea vikali.

“Nugu wewe, kwa nini unaniendea kinyume ilhali mimi ni jirani yako. Muda huo wote umekuwa ukimtongoza mume wangu na kuzuia penzi lake kwangu,” kipusa alimfokea mwenzake kwa hasira. Wawili hao walianza kurushiana cheche za matusi zilizoibua vita vikali.

“Lazima umkome mume wangu upende usipende. Na kwa taarifa yako utakiona cha mtema kuni,” kipusa aliendelea kufoka. Wapangaji kuona wawili hao wakimenyana waliingilia kati na kuzima mzozo huo ili kuepusha balaa.

Waliwakemea vikali vipusa hao kwa kuzua kisirani kwenye ploti huku wakimlaumu kipusa kwa kuvuruga ndoa ya mwenzake. Lakini mwanadada huyo alijigamba kuwa gwiji wa kuwaingiza boksi waume wa watu na kuwalaumu wanawake mtaani kwa kushindwa kuwaburudisha mabwana zao.

“Niacheni, ikiwa wanawake wameshindwa kuwatimizia waume zao hawafai kunilaunu nikijaza pengo hilo,” mwanadada aliwaeleza wapangaji na kuwaacha midomo wazi.