Habari Mseto

Nauli maradufu zawatatiza wanafunzi wakirudi shuleni

January 3rd, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

WAZAZI Alhamisi walitatizika kuwapeleka watoto wao shuleni licha ya walimu kufutilia mbali mgomo wao walivyoagizwa na mahakama.

Katika shule nyingi nchini, ni wanafunzi wachache waliofika kwa muhula wa kwanza wa mwaka huu baada ya wazazi kukwama magari yalipoongeza nauli maradufu.

Katika Kaunti ya Kisii, mabasi yalitoza nauli ya kati ya Sh1,500 na Sh2,000 hadi Nairobi badala ya Sh800.

Juliet Kwamboka na dada yake Janet Nyakerario, wanaosomea shule ya wasichana ya Pangani, walisema walifaa kuripoti shuleni jana, lakini walikosa usafiri.

Katika Kaunti ya Tana River, ni wanafunzi wachache waliofika shuleni kuanza masomo. Baadhi ya wanafunzi waliwasili shuleni saa tano za mchana na kusema walidhani walimu walikuwa wamegoma.

Wazazi katika kaunti hiyo walilalamika kwamba hawakuwa na pesa za kununulia watoto wao vifaa vya masomo.

“Nilipata mshahara Desemba 19 na ninatarajia kulipwa deni Januari 27. Sina pesa za kununua sare na vifaa vya masomo. Shule zingefunguliwa Januari 7 ili tupate muda wa kujipanga,” alisema Peninah Mwanza, mfanyakazi wa serikali.

Maafisa wa chama cha walimu katika kaunti hiyo waliwaagiza walimu kufika kazini. Katika Kaunti ya Mombasa, wanafunzi wengi walifika shuleni na walimu walikuwa kazini.

Hata hivyo, maafisa wa Knut walisema iwapo matakwa ya walimu hayatatimizwa, watagoma. Katika shule za Kaunti za Nyeri, Murang’a na Meru, walimu walifika kazini na kuwahudumia wanafunzi. Walimu wengi katika eneo hilo walisema hawakuwa tayari kugoma.

Katibu wa tawi la Murang’a Kusini, chama cha Knut, Bw John Njata alisema aliagiza walimu kujitokeza kazini.

Katika Kaunti ya Migori, walimu walifika kazini lakini ni wanafunzi wachache waliohudhuria masomo.

Katibu wa tawi la Migori la Knut Caleb Opondi alisema walimu waliamua kutii agizo la mahakama na wakasitisha mgomo. Mjini Migori, wanafunzi wengi walikwama vituo vya mabasi baada ya nauli kuongezwa maradufu.

“Wanafunzi wengi watachelewa kufika shuleni kwa sababu ya ukosefu wa usafiri. Sio vyema kufungua shule katikati ya wiki,” alilalamika mzazi John Omondi.

Hali ilikuwa hiyo hiyo katika Kaunti ya Kisumu huku wanafunzi wachache wakifika shuleni. Wazazi walisema waliamua kuwapeleka watoto wao shuleni Jumatatu ijayo.

Katika shule ya msingi ya Ayaro, Kisumu Mashariki, ni wanafunzi 100 waliofika miongoni mwa 420. Kulingana na mwalimu Mkuu Paul Odhiambo wazazi wengi hawajazoea shule kufunguliwa kati kati ya wiki.