Habari Mseto

Nauli yapanda shule zikifunguliwa

September 4th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

WAZAZI wiki hii hawana budi ila kutumia fedha zaidi kugharimia nauli kipindi hiki ambapo watoto wao wanarejea shuleni kwa muhula wa tatu na wa mwisho mwaka huu 2019.

Katika uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo mapema Jumanne na Jumatano katika steji kadhaa Nairobi, imebainika nauli kuelekea maeneo mbalimbali nchini imeongezeka mara dufu.

Magari yanayohudumu baina ya Nairobi, Nyeri, Karatina, Kirinyaga na Embu, abiria, wengi wakiwa wanafunzi walitozwa zaidi ya Sh500 kila mmoja.

Kwa kawaida nauli kuelekea maeneo hayo huwa kati ya Sh250 – 300.

Baadhi ya wazazi tuliozungumza nao walilalamikia ada hiyo ya juu, wakiiomba serikali kuidhibiti.

“Mtoto akirudi shuleni lazima karo ilipwe, mahitaji yake akiwa humo yananitegemea. Nauli ndiyo hiyo nayo imeongezwa. Gharama ya maisha imepanda; hizo pesa zote zitatoka wapi?” akashangaa mama mmoja aliyekuwa kituoni na mwanawe.

Taswira hiyo si tofauti na matatu zinazohudumu kati ya Nairobi, Nakuru, Eldoret, Nyanza na Magharibi mwa Kenya.

Walioelekea Nakuru mnamo Jumanne hawakuwa na budi ila kulipa nauli isiyopungua Sh500.

“Tunaotegemea magari ya umma hatuna la ziada ila kuitikia na sharti watoto warejee shuleni. Serikali inapaswa kudhibiti sekta ya usafiri na uchukuzi,” amependekeza mzazi.

Wahudumu tuliozungumza nao wamesema wenye matatu baada ya siku lazima wapate ‘mshahara’ na ndio maana wameongeza nauli.

Aidha, wengi wanashabikia ongezeko hilo, wanaoshawishi abiria kuingia kwenye matatu maarufu kama ‘Kamagera’ wakishika mateka stani zote ili kuhakikisha hakuna gari linalopunguza bei.

“Kahawa ikiiva lazima ichumwe,” akasema mmoja, akionekana kutania wasafiri.

Isitoshe, matatu zinazokusanya abiria njiani zinapakia kupita kiasi hasa magari ya Nairobi, Nyeri na Embu.

Kuondoa vizuizi

Miezi kadha iliyopita Inspekta Mkuu wa Polisi, IG, Hillary Mutyambai aliagiza maafisa wa trafiki nchini kuondoa vizuizi katika barabara zote nchini.

IG alisema vitakuwa vikiwekwa kupitia maelekezo ya kamanda wa kaunti, haja ikiibuka.

Ubebaji wa watu kupita kiasi ni suala hatari kwani baadhi ya madereva ni watepetevu pamoja na kuendesha kwa mwendo wa kasi.

Upandishaji wa nauli miongoni mwa wahudumu wa matatu nchini si jambo geni haswa baada ya likizo, wanafunzi wakirejea shuleni.

Msimu wa Krismasi wakazi wanaoishi mijini wakielekea mashambani kusherehekea na jamaa zao pia hawaepuki mjeledi wa nauli kuongezwa mara dufu. Hili hasa linatokana na utapeli wa wahudumu wa matatu, ambao tangu waziri wa usalama wa ndani Dkt Fred Matiang’i achukue usukani ameoneokana kushindwa kuwazima.