Nauli yapanda Wakenya wakirejea mijini

Nauli yapanda Wakenya wakirejea mijini

NICHOLAS KOMU NA SAMMY KIMATU

WAKENYA waliosafiri kwa sherehe za Krismasi wameanza kurejea mijini huku matatu zikiongeza nauli.Katika eneo la Kati, wengi waliamua kusafiri kwa kutumia gari la moshi lakini hilo halikuzuia matatu kuongeza nauli.

Nauli ya Sh200 kutoka Nanyuki hadi Nairobi kwa treni ilifanya watu zaidi ya 4000 kuitumia kurejea jijini.

Jana, Shirika la Reli lilitangaza kuwa litaongeza idadi ya treni kutoka Nanyuki hadi Nairobi ili kuhudumia idadi kubwa ya abiria inayoendelea kuongezeka tangu Disemba 12 huduma hizo ziliporejelewa baada ya kusitishwa kwa miaka miwili.

Treni hiyo ilijaa hadi abiria wakasimama na wengine kuketi kwenye sakafu.Mwenyekiti wa chama cha wamiliki wa matatu eneo la Mlima Kenya, Michael Kariuki alisema nauli nafuu inayotozwa na treni ni pigo kwa biashara ya matatu. Matatu zilitoza nauli ya kati ya Sh700 na Sh1000 huku treni ikitoza Sh200 kutoka Nanyuki hadi Nairobi.

Bw Kariuki alisema walilazimika kuongeza nauli kwa sababu wanabeba abiria wachache ili kuzingatia kanuni za kuzuia kusambaa kwa corona.

“Ni kweli tunapoteza biashara kwa kuwa watu wengi wanakimbilia treni kwa sababu ya nauli ya chini. Kufufuliwa kwa reli ni jambo nzuri kwa uchumi lakini kunafaa kuwa na usawa katika biashara hasa katika nauli,” alisema Bw Kariuki.

Jana, treni iliyokuwa ikielekea Nairobi ilikwama kwa muda eneo la Ruthagati, Kaunti ya Nyeri. Nauli ilipanda kwa asilimia 100 kutoka Nairobi hadi Machakos wahudumu wa matatu wakisema kuna idadi kubwa ya watu wanaorejea kazini.

Katika kaunti ya Murang’a, hali ilikuwa sawa jana matatu zilipoongeza nauli kwa kati ya asilimia 50 na 100.Wahudumu wa matatu walisema huenda nauli isishuke hadi wiki kati kati ya Januari mwaka ujao baada ya wanafunzi kurejea shuleni. Shule zitaanza kufunguliwa Januari 4.

You can share this post!

Wasichana wakeketwa na kuozwa Baringo

CORONA: Shule bado kujiandaa