Habari Mseto

Nawazia kumfichulia jirani vile mkewe anamcheza

January 26th, 2024 1 min read

SHANGAZI

Kwako shangazi? Mwanamke jirani yangu amekuwa akileta mwanamume mpenzi wake nyumbani kwao mumewe akiwa kazini. Ni marafiki zetu na nahisi vibaya kuhusu tabia yake hiyo. Nafikiria kumwambia mume wake. Waonaje?

Mwanamke huyo hastahili ndoa. Ukimwambia mumewe kuhusu yanayoendelea nyumbani kwake, huo utakuwa mwisho wa ndoa yao na mwanamke huyo atakulaumu wewe. Badala yake, jaribu kumwelezea hatari iliyopo uone kama atabadilika.

Amenitumia picha akila fuska na mke wangu, naumia, nahisi kumuua

Nimeajiriwa na ninafanya kazi mbali na nyumbani. Kuna mwanamume nisiyemjua ambaye alinitumia picha zake na mke wangu wakila mahaba chumbani. Nafikiria kuua mtu. Nahitaji ushauri wako.

Kama umethibitisha picha ulizotumiwa ni za mke wako, sasa umejua si mwaminifu kwako. Lakini kumbuka kuua ni hatia. Ndoa si kifungo cha maisha. Watu huoana na kuachana kwa sababu nyingi. Usifungwe jela kwa ajili yake, achana mke wako na uanze maisha upya.

Mke wa jirani sasa ataka kulipa deni kwa mapenzi

Jirani yangu aliniomba pesa miezi mitatu iliyopita na kufikia sasa hajanilipa. Juzi alinitumia ujumbe kwa simu akaniambia anataka kunilipa kwa mapenzi. Ni mke wa mtu na sitaki balaa. Nifanyeje?

Inawezekana mwanamke huyo amekosa pesa ama anahisi vigumu kukulipa na ameamua kutumia njia hiyo haramu kumaliza deni. Inawezekana pia anakupenda na anatumia deni hilo kama njia ya kukunasa. Usikubali. Akishindwa kukulipa pesa zako achana naye tu.

Ex wa mume wangu haachi kumpigia simu kuhusu mtoto wao

Mwanamke aliyezaa na mume wangu kabla hajanioa amekuwa akimpigia simu kuhusu mtoto huyo. Nahofia atatumia nafasi hiyo kumnasa tena na nafikiria kumchukua mtoto huyo ili kuvunja uhusiano wao. Nishauri.

Huwezi kumchukua mtoto huyo bila idhini ya mama yake. Ni kweli mwanamke huyo anaweza kutumia mtoto kufufua uhusiano kati yao. Lakini hilo litawezekana tu kama mume wako si mwaminifu kwako. Kuwa macho.