Kimataifa

‘Nchi nyingi hazithamini usalama wa wahamiaji na watafuta hifadhi’

September 24th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

WASHINGTON D.C., Amerika

DUNIA inaendelea kuwa hatari kwa wahamiaji na watafuta hifadhi kutoka sehemu mbalimbali, umeonyesha utafiti mpya.

Ripoti ya utafiti huo ambayo ilitolewa Jumatano na shirika la Gallup, unaonyesha kuwa nchi nyingi zinaendelea kuweka vikwazo ili kutowaruhusu wahamiaji kutafuta hifadhi, huku mazingira wanakopewa hifadhi yakiwa si salama.

Hilo linajiri huku Ulaya jana ikizindua mpango mpya kuhusu wahamiaji, baada ya moto mkubwa kutokea kwenye kambi yao moja nchini Ugiriki na kuwaacha maelfu ya watu bila makao.

Ripoti ilizitaja nchi za Macedonia Kaskazini, Hungary, Serbia na Croatia kuwa miongoni mwa zile zimeweka kanuni kali zinazowazuia wahamiaji kuingia huko.

Hata hivyo, baadhi ya nchi bado zinaendelea kuwapa hifadhi wahamiaji wanaotoroka mizozo kwenye mataifa yao, ikilinganishwa na sera zake kali hapo awali.

Baadhi ya mataifa hayo ni Peru, Equador na Colombia. Nchi hizo zimekuwa zikiwapokea maelfu ya wahamiaji wanaotoroka mzozo wa kisiasa nchini Venezuela.

Nchi zilizoorodheshwa kuwapokea wahamiaji bila vikwazo ni Canada, Iceland na New Zealand.

Watu zaidi ya 140,000 walihojiwa katika nchi na maeneo 145 kote duniani.

Utafiti ulihusisha kuwauliza watu jinsi walivyohisi kuhusu uwepo wa wahamiaji katika nchi zao, kuwa majirani nao au hata kuoana nao.

Mtaalamu wa masuala ya uhamiaji katika shirika hilo, Julie Ray, alisema kuwa kiwango cha kukubaliwa kwa wahamiaji kilishuka kutoka 5.34 mnamo 2016 hadi katika kiwango cha 5.21 mwaka uliopita. Mtaalamu huyo alisema hali hiyo imechangiwa na mabadiliko kwenye sera za kisiasa na kiutawala kwenye baadhi ya nchi.

Kiwango hicho kilishuka nchini Peru kutoka 6.33 mnamo 2016 hadi 3.66 mwaka uliopita, huku idadi ya watu walioridhishwa hali ya wakimbizi kuwepo nchini mwao Colombia ikishuka kutoka asilimia 61 mnamo 2016 hadi asilimia 29 pekee mwaka 2019.

Shirika hilo lilifanya utafiti wa kwanza mnamo 2015 baada ya zaidi ya watu milioni moja kusafiri katika mataifa mbalimbali barani Ulaya kutafuta hifadhi kutokana na migogoro ya kisiasa. Idadi kubwa ya wahamiaji hao walitoka Afrika na eneo la Mashariki ya Kati.

Wataalamu wa uhamiaji wameutaja mwelekeo huo kuwa hatari, hasa kwa wahamiaji wanaotafuta hifadhi katika nchi za Ulaya kutoka Afrika.

Mamia ya wahamiaji wamekuwa wakifariki kila mwaka katika Bahari ya Mediterranean, wakijaribu kutafuta njia za mkato kutafuta hifadhi Ulaya. Mataifa ya Ulaya yamekuwa kwenye mzozo wa muda mrefu baina yao kuhusu vile yatadhibiti ongezeko la wahamiaji hao.