Habari

Nchi ya wakora

October 19th, 2019 3 min read

Na WAANDISHI WETU

KATIKA siku za hivi karibuni, Wakenya wamekuwa wakipoteza pesa na mali yao mikononi mwa matapeli wa aina mbalimbali, baadhi yao wakilenga kushirikiana na serikali au kuingia ndani yake.

Uchunguzi wa mashirika mbalimbali yakijumuisha bunge, umebaini kuwa utapeli huo umekita mizizi katika asasi za umma, maafisa wakipanga jinsi ya kutumia njia za mkato kujipatia utajiri wa haraka na kuwaacha maskini wakiteseka.

Uchunguzi unaoendeshwa na bunge la seneti kuhusu Mpango wa Serikali Kuu wa Ukodishaji wa Vifaa vya Matibabu (MES) kwa hospitali za kaunti, umefichua kuwa umma umekuwa ukitapeliwa pakubwa. Pesa zilizotengewa serikali za kaunti kutoka kwa mfuko wa umma zimetumika kulipia vifaa vya matibabu ambavyo vinaweza kununuliwa kwa bei nafuu katika soko huru.

Kwa mfano, wanachama wa kamati ya seneti inayochunguza ikiwa pesa za umma zilitumiwa ipasavyo katika mradi huo wa takriban Sh39 bilioni, walielezwa kuwa vifaa kama troli na glavu zilikodishwa kwa bei ya juu kuliko bei ya kuzinunua katika soko huru.

Ulaghai kama huo ulifichuliwa wiki hii katika Hazina ya Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) baada ya kuibuka kuwa baadhi ya pesa hazikuwa zikiingia katika akaunti ya shirika hilo. Hii ilifanya wanachama wengi kukosa kunufaika na bima hiyo licha ya kutumia nambari za M-Pesa zilizotolewa na hazina hiyo.

Visa vimeripotiwa vya Wakenya kutapeliwa mamilioni ya pesa kupitia vyeti feki vya ardhi. Wiki jana, polisi katika Kaunti ya Bomet walifichua sakata ya uchapishaji na utoaji hatimiliki za mashamba ambazo ni feki.

Mshukiwa Leonard Kipkoech almaarufu Marekete, ambaye ni Soroveya wa kibinafsi, alikamtwa kwa kutoa hati hizo bandia kwa watu 13 walionunua ardhi katika eneo la Sotik. Polisi walisema wanashuku sakata hiyo imekuwa ikiendelezwa kwa usaidizi wa maafisa wa ardhi katika afisa za wizara ya ardhi mjini Bomet.

“Tunaendelea na uchunguzi kwa lengo la kuwakamata maafisa wa wizara ya ardhi ambao hushirikiana na tapeli huyu kuwapunja wananchi wasio na ufahamu,” akasema Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Bomet Naomi Ichami.

Duru zilisema soroveya huyo huwatoza wateja wake kati ya Sh20,000 na 40,000 kila mmoja akipewa hatimiliki ya shamba. Polisi walimpata Bw Marekete na hatimiliki tisa lakini walipofanya msako nyumbani kwake wakapata nyingine nne.

Uchunguzi kuhusu sakata hiyo ulianzishwa baada ya wananchi kuwasilisha malalamishi kwa polisi kuhusu utapeli huo.

Katika msitu wa Mau ambako wanaokaa hapo kinyume cha sheria wanafurushwa, serikali ilisema baadhi ya vyeti vilikuwa feki.

Sakata hiyo ilifichuliwa mwezi mmoja baada ya serikali ya kitaifa kuanza kutekeleza awamu ya pili ya ufurushaji wa walowezi katika Msitu wa Maasai katika kaunti jirani ya Narok.

Inasemekana kuwa baadhi ya familia hizo 6,000 zilipewa hatimiliki feki baada ya kuuziwa ardhi katika msitu huo ambao ni mojawapo ya chemchemi tano kuu za maji nchini.

Utapeli sekta ya afya

Utapeli huu umeenea katika sekta ya afya huku uchunguzi wa hivi punde ukibaini kuwa zaidi ya taasisi 800 za afya, za umma na kibinafsi, zimekuwa zikihudumu bila kuzingatia kanuni zilizofaa. Kaimu Mkurugenzi wa Afya Wekesa Masasabi aliamuru kufungwa kwa vituo hivyo na kutwaliwa kwa leseni zao za kuhudumu.

“Ukaguzi ambao uliendeshwa kuanzia Februari hadi Agosti 2019 umefichua kuwa jumla ya vituo 811 vya afya kote nchini havijatimiza viwango vinavyohitajika. Kwa mfano, havina wahudumu waliohitimu, miundomsingi na vifaa vya kimsingi vinavyohitajika kulingana na sheria ya madaktari na wataalamu wa meno (MPDB). Kwa hivyo, tumeamuru vituo hivi vifungwe kwa kuwatapeli wananchi huku vikihatarisha maisha yao,” akasema.

Miongoni mwa vituo vilivyofungwa, 92 vinapatikana Nairobi, 34 Nyanza, Mombasa 98, Kiambu 46, Murang’a 43, kati ya maeneo mengine.

Dkt Masasabi aliongeza kuwa uchunguzi huo uligundua kuwa wengi wa wahudumu wa afya wanaofanya kazi hawajahitimu.

Utapeli mwingine unahusu idara ya usalama. Maafisa wa polisi, ambao wanapaswa kuwalinda raia wamegeuka kuwa maadui wakubwa huku wakihusishwa na visa kadhaa vya wizi.

Baadhi ya watu wamekuwa wakiwatapeli watu pesa na kuwapa leseni feki za kuendesha magari, vyeti bandia vya bima na vya kuzaliwa.

Ijumaa, mwanamume alishtakiwa kwa kupatikana na vyeti 38 feki vya kuzaliwa.