NCIC yaonya wanasiasa wasiotaka kuona washindani ngomeni

NCIC yaonya wanasiasa wasiotaka kuona washindani ngomeni

Na CHARLES WASONGA

TUME ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) imewaonya wanasiasa dhidi ya kuwazuia mahasidi wao kuingia katika maeneo wanakotoka.

Kwenye taarifa aliyoituma kwa vyombo vya habari Jumanne, mwenyekiti wa tume hiyo Samuel Kobia alisema mwenendo kama huo unaweza kuchochea hatua za kulipiza kisasi na hivyo kusababisha fujo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

“NCIC imeghadhabishwa na ongezeko la visa ambapo wanasiasa wamezuiliwa kuzuru maeneo fulani eti kwa sababu ni ngome ya wanasiasa wengine ambao hawaelewani nao. Vitendo kama hivi vikome kabisa kwa sababu vinaweza kusababisha ghasia wakati kama huu tunapoelekea uchaguzi mkuu,” Dkt Kobia akasema.

Onyo hilo limejiri siku mbili baada ya wafuasi wa Naibu Rais William Ruto kumlaumu Mbunge wa Kieni Kanini Kega kufuatia vurugu zilizozuka Jumapili wakati Dkt Ruto alihudhuria ibada ya Jumapili eneo hilo.

Makundi ya watu waliodaiwa kukodiwa na Bw Kega waliwazomea wanasiasa wandani wa Dkt Ruto, kiongozi huyo alipohudhuria ibada katika Kanisa la PAG, eneo la Mbiriri, eneobunge la Kieni.

Hata hivyo, Dkt Ruto na wabunge wapatao 40 wanaoegemea chama cha United Democratic Alliance (UDA) walihudhuria ibada hiyo katika kanisa hilo lililojengwa kwa mabati.

Ingawa hivyo, Jumanne, Dkt Kobia hakurejelea tukio hilo katika taarifa yake.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo alitaja kisa cha Januari 2021 ambapo Seneta wa Baringo Gideon Moi alizuiwa na kundi la vijana kuzuru eneo fulani katika Kaunti ya Nandi kwa shughuli fulani za kitamaduni.

Katika mwezi huo, patashika ilizuka katika eneo la Githurai wakati wa ziara ya kiongozi wa ODM Raila Odinga katika eneo hilo ambapo watu waliodaiwa kuwa wafuasi wa Dkt Ruto walijaribu kuvuruga ziara hiyo.

“NCIC ingependa kuwakumbusha Wakenya kwamba wanasiasa wote wanakubalika kunadi sera zao katika sehemu mbali mbali nchini. Hakuna mwanasiasa aliye na kibali cha kuzuia mwenzake, wanayetofautiana kimawazo, kuzuru sehemu yoyote nchini,” akasisitiza Dkt Kobia.

“Tutawafungulia mashtaka wanasiasa ambao watajifanya eti wanazuia washindani wao kuzuru ngome zao. Kenya ni moja, na hakuna mwanasiasa anayemiliki eneo lolote nchini,” akaongeza.

Dkt Kobia pia alitangaza kuwa hivi karibuni tume ya NCIC itazindua mpango wake kuhusu matayarisho ya uchaguzi mkuu usio na fujo na ghasia. Mpango huo utajulikana kama ‘Roadmap to Elections Bila Noma’.

You can share this post!

AKILIMALI: Unavyoweza kudumisha rutuba ya udongo kwa...

Muuzaji bidhaa za hospitali apewa muda kulipa deni la...