Habari Mseto

NCIC yapendekeza wanasiasa wachochezi wazimwe uwaniaji

September 11th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE ambao watakuwa wameshtakiwa kwa kosa la kutoa matamshi ya chuki huenda wakazuiwa kushiriki uchaguzi mkuu wa 2022 endapo mabadiliko ya sheria yanayopendekezwa na Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) yatapitishwa bungeni.

Kamishna wa tume hiyo Sam Kona alisema Alhamisi jioni kuwa tume hiyo imependekeza sheria yake ifanyiwe mabadiliko ili iwe mojawapo ya asasi za kuwaidhinisha wagombeaji nyadhifa za kisiasa.

“Tayari tumependekeza kuwa mtu yeyote ambaye atashtakiwa mahakamani kwa kosa la kuchochea chuki na uhasama kupitia matamshi yake, azimwe kugombea wadhifa wote wa kisiasa. Mtu kama huyo atazuiwa viti kama vile Urais, Ugavana, Useneta, Ubunge na Udiwani,” akasema Bw Kona kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen.

Ilivyo sasa ni kwamba Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA), Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Bodi ya Kutoa Mkopo kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (HELB) na Asasi ya Kuandamana Waliofeli kulipa Madeni (CRB) ndio huwapiga msasa wagombeaji kubaini kama wanafaa kugombea viti vyote sita.

Baadaye Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) huthitibitisha na kuidhinisha kwamba mtu huyo anafaa kugombea.

NCIC sio mojawapo ya asasi za kuwapiga msasa wagombeaji.

Pendekezo hilo limejiri wakati ambapo wabunge Johanna Ng’eno (Emurua Dikirr) na Oscar Sudi (Kapseret) wameelekezewa shutuma kali kwa kile wakosoaji wanasema ni kumkosea heshima Rais Uhuru Kenyatta na mamake, Mama Ngina Kenyatta.

Mnamo Alhamisi Rais Kenyatta pia alitoa kauli kukemea wenye tabia ya kumkebehu mamake.

Bw Ng’eno aliwasilishwa mahakamani Nakuru na kushtakiwa kwa kosa la kutoa matamshi ya chuki ambayo yanaweza kusababisha ghasia na umwagikaji wa damu.

Aliachiliwa huru Alhamisi, Septemba 10, 2020, kwa dhamana ya Sh2 milioni na kesi yake ikapangiwa kusikizwa mnamo Septemba 27, 2020.

Hata hivyo, Bw Sudi hajakamatwa. Lakini ameshikilia kuwa hakufanya kosa lolote na hawezi kumwomba msamaha Rais Kenyatta na familia yake.

Wanasiasa ambao wamewahi kufikishwa mahakamani kwa kosa la kutoa matamshi ya chuki wabunge; Junet Mohammed (Suna Mashariki), Florence Mutua (Busia), Moses Kuria (Gatundu Kusini), Kimani Ngunjiri (Bahati) miongoni mwa wengine.

Ikiwa mabadiliko ya sheria yanayopendekezwa na NCIC yatapitishwa wabunge hawa na wanasiasa wengine kama vile Seneta wa zamani wa Machakos watazimwa kushiriki uchaguzi mkuu wa 2022.