NCIC yashtakiwa kuhusu sipangwingwi

NCIC yashtakiwa kuhusu sipangwingwi

Na RICHARD MUNGUTI

VUGUVUGU la mawakili wamewasilisha kesi katika mahakama kuu kupinga marafuku ya matumizi ya maneno “hatupangwingwi na watajua hawajui.”

Kupitia kwa mawakili Felix Kiprono na Vincent Yegon , Chama cha Mawakili Limited (CML) kinaomba mahakama kuu ifutilie mbali marufuku iliyotolewa na tume ya uuwiano na utangamano wa kitaifa (NCIC) dhidi ya matumizi ya maneno hayo. Maneno haya yamo katika wimbo uliotungwa na mwanamuziki Tonny Kinyanjui almaarufu Exray anayemshikirisha Naibu wa Rais William Ruto.

Katika wimbo huo Dkt Ruto ananukuliwa akisema,”kama vile wakenya wanasema hawapangwingwi hata mimi kama hasla nasema sipangwingwi.” Mawakili Kiprono na Yegon wameeleza katika kesi waliyoshtaki kwamba maneno hayo hayaashirii chuki ama uchochezi.

Chama hiki cha mawakili kimedai NCIC inatumia mamlaka yake vibaya kukandamiza haki za wananchi kufurahia uhuru wa usemi. CML kinaomba mahakama kuu itumie mamlaka yake kutafsiri maneno haya yaliyotangazwa na NCIC mnamo Aprili 8,2022 kuwa ya uchochezi na kueneza hisia za kikabila.

Wanaomba mahakama kuu izuie NCIC kuwachukulia hatua za kisheria wanasiasa ama wanamuziki ambao watayatumia. “Tume ya NCIC imejiingiza katika ulingo wa siasa na kuacha majukumu iliyobuniwa,” Bw Kiprono amesema katika ushahidi aliowasilisha mahakamani.

Bw Kiprono ameomba mahakama kuu ipokee kesi hiyo na kuiratibisha kuwa ya dharura na kutoa maagizo kabla ya NCIC kuanza kuwakamata wakenya watakaotumia maneno hayo na kuwashtaki mahakamani. Kesi hiyo iliwasilishwa mbele ya Jaji Antony Ndung’u kutolewa maagizo.

You can share this post!

Sitaki kingine ila mchujo, Shahbal akaa ngumu ODM

Base Titanium yasifiwa kwa kuwezesha jamii

T L