Habari Mseto

NCIC yashtumu fujo zilizoua wawili Murang’a

October 6th, 2020 1 min read

Na JUMA NAMLOLA

TUME ya Uwiano na Utangamano (NCIC), inataka polisi wachunguze na kuwakamata watu waliohusika katika ghasia katika Kaunti ya Murang’a, ambapo watu wawili waliaga dunia.

Mwenyekiti wa NCIC, Dkt Samuel Kobia, alisema kwenye taarifa kwamba wakuu wa usalama wanapaswa kuzuia nchi kujikuta ilipokuwa 2007.

“Hatutakubali mijadala itakayotuingiza katika kampeni za mapema. Tunasisitiza kwamba ni lazima vyama vyote vya kisiasa vitambue haki ya kila Mkenya. Haki ya uhai, haki ya kujieleza, haki ya kuwa huru na haki ya kufurahia mazuri yote yaliyoletwa na Katiba,” akasema.

Alieleza masikitiko ya tume yake kwamba wanasiasa wameanzisha mjadala wa wanaojiita ‘mahasla’ na ‘koo za kifalme’ kwa njia inayoweza kuelekeza nchi katika mauaji ya halaiki kama yaliyotokea Rwanda mnamo 1994.

Tume hiyo inasema haitavumilia chuki kuzagaa nchini, ikiwa imesalia karibu miaka miwili kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.