NCPB yaahidi kuboresha huduma kwa wakulima wa mahindi

NCPB yaahidi kuboresha huduma kwa wakulima wa mahindi

NA RICHARD MAOSI

Ni habari njema kwa wakulima wa mahindi katika eneo la Bonde la Ufa baada ya Bodi ya Kitaifa ya Mazao na Nafaka (NCPB), kusema haitakuwa ikichukua mahindi kutoka kwa wakulima kwa deni.

“Baada ya kufanya majadiliano ya kina na washikadau, tumegundua wakulima wengi wamekuwa wakipata hasara miaka ya mbeleni baada ya kusambaza mahindi, lakini baadaye malipo yakaishia kwa mifuko ya watu wachache,” akasema mwenyekiti wa NCPB Mutea Iringo ambaye alizuru Kaunti ya Nakuru, Jumatatu kutathmini ubora wa eneo hilo la kuhifadhia nafaka.

Alieleza kuwa visa vya ufisadi na ubadhirifu wa hela za wakulima ni miongoni mwa mambo ambayo serikali imepiga msasa, ambapo alikiri kuwa tangu sasa wakulima watakua wakipokea malipo yao kwenye benki.

Aidha Iringo aliongezea kuwa gharama ya kuhifadhi gunia moja la mahindi imeshuka kutoka Sh 10 hadi shilingi tatu, akiwaomba wakulima kutumia fursa hii kuhakikisha nafaka zao zinadumisha ubora wa hali ya juu.

Shughuli ya kupakia na kupakua shehena ya mahindi kutoka kwa wakulima. Picha/Richard Maosi.

“Ikumbukwe kuwa kufikia sasa serikali imenunua zaidi ya magunia 650,000 ya mahindi na bado tutaendelea kununua,”aliongezea.

Vilevile NCPB inashirikiana na Chuo Kikuu Cha Embu kwa kuwapatia wakulima wa mahindi ushauri wa kitaaluma, ili kupiga jeki mazao yao yakiwa shambani , mbinu za kupalilia, kupanda na kuvuna..

Aidha Shirika la Kenya Agricultural and Livestock Research Organisation(KALRO) wanashirikiana na wakulima kubaini spishi mbalimbali za mahindi ambazo zinaweza kufanya vyema kwenye mazingira mbalimbali.

Kwa upande mwingine Peter Chege ambaye ni msemaji wa wakulima alisema bodi imekuwa ikiwakandamiza wakulima kwa kuweka kiwango cha mahindi ya kusambaza.

Alisema kuwa mara nyingi wakulima wamekuwa wakishauriwa wasisambaze zaidi ya gunia 1000 ya kilo 90 ya mahindi. PICHA/ RICHARD MAOSI

Aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa uwezo wa wakulima kukuza mahindi hautoshani, na mwaka huu mazao ni mengi.

Chege aliunga mkono hatua ya serikali ya kupiga marufuku mahindi kutoka nje ya nchi, akisema kuwa itasaidia kutengeneza bei na kupanua soko.

Hata hivyo, aliomba serikali kuongeza bei ya mfuko mmoja wa kilo 90 kutoka Sh2,700 hadi Sh3,000, kwa sababu bei ya mafuta imepanda.

 

You can share this post!

Aunda programu za kompyuta kuifaa mikahawa

Mawakili wamtoroka Sonko ‘apambane na hali yake’