Habari Mseto

NCPB yatumia Sh6.8 bilioni kununua mahindi

March 12th, 2019 1 min read

NA BARNABAS BII

BODI ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB)  imetumia Sh6.8 bilioni kununua magunia 270,000 ya mahindi huku wakulima wengi wakiendelea kujitayarisha kwa msimu mpya wa upanzi kwa kununua pembejeo za kilimo.

NCPB ilinunua magunia 240,000 zenye thamani ya Sh6 bilioni kutoka kwa wakulima Kaskazini mwa Bonde la Ufa baada ya Hazina ya Uhifadhi wa Chakula (SFRTF) kutoa Sh4 bilioni kuwalipa wakulima waliowasilisha mazao yao kwa bodi hiyo.

Mwenyekiti wa SFRTF Dkt Noah Wekesa, alisema malipo kwa wakulima imekuwa ikendelea vyema baada ya wao wenyewe kupitia mchakato wa kina wa ukaguzi ulioendeshwa na kamati iliyobuniwa ya wakaguzi.

Kulingana na Dkt Wekesa, zaidi ya wakulima 400 walioidhinishwa walilipwa wiki jana wakati milolongo mirefu ikiendelea kushuhudia kwenye mabohari mbalimbali ya NCPB, wakulima wakiwa mbioni kuyauza mahindi yao ili kupata fedha za kununua pembejeo za kilimo.

“Tumenunua kiasi kikubwa cha mahindi kwenye mabohari ya Eldoret, Kitale, Moi’s Bridge na Ziwa. Hata hivyo, wakulima bado hawajaidhinishwa kupokea malipo yao katika mabohari mengine,” akasema Meneja wa Mawasiliano wa NCPB Titus Maiyo.

Aidha, alifichua kwamba NCPB ilitumia Sh200 milioni zilizopokea kutoka kwa SFRTF wiki jana kuwalipa wakulima kutoka Kaskazini mwa Bonde la Ufa, ambao ndio huzalisha kiasi kikubwa mahindi yanayotumika nchini.

“Tunatarajia kupokea pesa zaidi kutoka kwa SFRTF kugharimia malipo ya wakulima waliowasilisha mazao yao kwa NCPB kati ya Februari 18 hadi Marchi 2,” akaongeza Bw Maiyo.

Serikali inapanga kuyanunua magunia 2 milioni yenye thamani ya Sh5 bilioni kwa Sh2,500 kwa kila gunia la kilo 90 kutoka kwa Sh2,300 ya iliyokuwa imependekezwa mwaka jana.

Hata hivyo, masharti makali ya ukaguzi yamechangia wakulima wengi kuchelea kuwasilisha mahindi yao kwa NCPB huku bodi yenyewe ikilalamikia uhaba wa magunia ya kuyahifadhi mahindi hayo.

“Tunairai serikali kulegeza baadhi ya masharti magumu yatakayopelekea wakulima kupata hasara,” akasema mkulima Noah Too akiwa kwenye foleni Eldoret.