Kimataifa

Ndani kwa kuchoma nyumba ya mpenzi wa zamani akitaka warudiane

January 14th, 2019 2 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAFUNZI mmoja kutoka Uingereza alifungwa miaka sita gerezani, baada ya kuteketeza nyumba ya aliyekuwa mpenzi wake, akitaka warudiane.

Conor Egan wa miaka 20 alidaiwa kusukuma magurudumu ya majaa ya taka yaliyokuwa na moto kuelekea mlango wa Phoebe Alton, akilenga kuwa kisa hicho kingemtisha na kumfanya kumrudia baada yao kuachana.

Korti moja ya Chester ilifahamishwa kuwa uhusiano baina ya wawili hao ulivunjika walipokuwa katika chuo kikuu, japo Egan alikuwa akimtaka Alton na alitaka warudiane.

Alisemekana kuwahi kujaribu mbinu hyo tena mnamo Mei mwaka uliopita alipoanzisha moto katika mtaa wa Lone Street ‘akitaka kupendwa na Alton tena.’

Ilidaiwa kuwa alitarajia kuwa baada ya kuteseka, msichana huyo angefika kwake akitaka kutulizwa na mahali pa kuishi, japo bila kujua kuwa ni yeye aliyeanzisha shida hiyo.

Jumatatu, Egan alifungwa miaka sita gerezani na kuzuiwa na korti kuwahi kuzungumza na Alton. Jaji Steven Everett alisema kesi hiyo inafaa kushughulikiwa kwa umakinifu kwani kuteketeza kunaweza kusababisha kifo.

“Moto ni kitu kigumu kuzuia kwani ukianza kuteketeza unasababisha hasara ya mali na maisha na ndipo vifungo vya kuanzisha moto ni vikali. Sifurahii kuona mwanaume mchanga kama wewe akijiharibia maisha kama jinsi umefanya lakini baada ya kutoka gerezani tutaona ikiwa utakuwa umerekebika,” jaji akamweleza mshtakiwa.

Kiongozi wa mashtaka alieleza korti wawili hao walianza uhusiano Oktoba 2017 lakini baada ya krismasi ya mwaka huo wakaanza kukosa kuonana wakati mwingi, licha ya juhudi za Egan kutaka uhusiano huo ushike mizizi kabisa.

Mwanaume huyo alidaiwa kuanzisha moto katika nyumba ya Alton mara mbili mnamo Mei mwaka uliopita. Ilibidi polisi na wazima moto kufika ili kuizima.

Egan alianza kushukiwa wakati Alton alimpigia simu kumfahamisha kuhusu matukio hayo, naye kwa pupa akajitetea kuwa hakufanya hivyo.

Hata hivyo, mashahidi walisema waliona mwanaume akitoka katika eneo la nyumba ya Alton, na mavazi waliyoeleza yakawa ya Egan.

Simu yake ilipochunguzwa, ilibainika kuwa hakuwa amelala wakati wa mioto hiyo kama alivyosema.

Alipokamatwa, alikana kuanzisha mioto hiyo, lakini baadaye akakiri makosa hayo.

Jamaa huyo aliyekuwa akisomea kuwa mwalimu wa shule ya msingi katika chuo kikuu baadaye alitimuliwa chuoni.

Alipotekeleza kosa hilo, Egan alikuwa na miaka 19. “Alifanya hivyo kutokana na hali ya kukosa ukomavu na kushindwa kukubali kuwa uhusiano ulikuwa umeisha. Haikuwa ulipizaji kisasi bali kuvuta mapenzi,” akasema wakili wake.