Habari Mseto

Ndani kwa kuiba nguruwe wa thamani ya Sh400,000

June 19th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MAHAKAMA ya Kibera Jumatano ilimfunga miaka miwili jela mwanamume aliyeiba nguruwe ili kumfurahisha mpenzi wake. 

Stephen Nderitu ambaye alikuwa ameajiriwa kuwalisha nguruwe hao 18 alidaiwa kuwaiba mnamo Julai 22, 2018, kisha akatorokea nyumbani kwa mpenzi wake Nakuru kujificha.

Korti ilielezwa kuwa mwajiri wa Bw Nderitu Kennedy Wangila alikuwa ametoka nyumbani kwenda kununulia mwanawe viatu na akawaacha wanyama hao wakila, lakini alipofika akawakosa.

Baadaye aliambiwa na majirani kuwa mshukiwa alifika na lori na akawabeba nguruwe wote, waliokuwa wa thamani ya Sh400,000.

Akitoa uamuzi, Hakimu Mkuu Mkazi katika mahakama ya Kibera Boaz Ombewa alisema upande wa mashtaka ulidhihirisha kuwa Bw Nderitu aliiba nguruwe hao.

Upande wa mashtaka uliwaita mashahidi wanne mbele ya korti.

Mshukiwa anadaiwa kuwa aliwauza wanyama hao katika kichinjio kimoja eneo la Ndumberi, kabla ya kutorokea kwa mpenzi wake Nakuru.

Mshukiwa, hata hivyo alipinga kosa hilo na kudai kuwa mwajiri wake ndiye aliwaiba nguruwe hao. Alieleza korti kuwa amekuwa mfanyakazi mtiifu aliyemfanyia mwajiri wake kazi tangu 2017.

Alihukumiwa miaka miwili jela, au alipe faini ya Sh300,000.