Habari Mseto

Ndani kwa kumbaka na kumwambukiza mpwa HIV

September 27th, 2018 1 min read

Na VITALIS KIMUTAI

MLINZI mmoja ameshtakiwa katika mahakama moja ya Bomet kwa kumwambukiza mpwawe virusi vya Ukimwi kimakusudi.

Mshtakiwa, Reuben Kipng’etich, mwenye umri wa miaka 37 pia anakabiliwa na shtaka la kufanya mapenzi na mtoto huyo ambaye ni jamaa yake.

Akiwa mbele ya Hakimu Mkuu Pamela Achieng’, alishtakiwa kwamba mnamo Septemba 19 katika kijiji cha Tendwet, Kata ya Chemaner, Kaunti ya Bomet alifanya kitendo hicho kinyume cha sehemu 20 (1) ya Sheria kuhusu Ngono, ya mwaka 2006.

“Licha ya kufahamu kwamba ana virusi vya Ukimwi, alifanya mapenzi kimakusudi na mwathiriwa ambapo alimwambukiza,” likaeleza shtaka .

Hata hivyo, mshtakiwa alikana mashtaka hayo ambapo hakimu aliagiza aachiliwe kwa dhamana ya Sh100,000 pesa taslimu na mdhamini wa kiasi kama hicho.

Mshukiwa anahudumu kama mlinzi katika Kaunti ya Machakos.

Hata hivyo, alishindwa kutoa dhamana hiyo, hali iliyomfanya kuwekwa rumande katika gereza la Serikali la Kericho akingojea kesi hiyo kusikizwa tena hapo Oktoba 30 mwaka huu.

Mshtakiwa alikamatwa baada ya kudaiwa kuvunja nyumba ambayo mtoto huyo alikuwa amelala katika makazi ya wazazi wake. Mwathiriwa alikuwa amelala chumbani humo na dada yake mdogo.

Chifu wa eneo hilo David Kebenei aliwaambia wanahabari kwamba wakati alipokamatwa, mshukiwa alikuwa akijaribu kutoroka. Chifu huyo alisema mshtakiwa alifika kwao majuzi kutoka anakofanya kazi kuhudhuria mazishi ya ndugu yake mdogo ambaye alijiua baada ya kumuua mpenziwe.

Inadaiwa kwamba marehemu alidunga kisu mpenziwe baada ya kukataa onbi lake la kutaka kumwoa.

Alitambuliwa kama David Saina, mwenye umri wa miaka 38 huku mwanamke akitambuliwa kama Winny Chelagat wa miaka 24. Mwanamke huyo alikuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Kabianga.