Ndani miaka 10 kwa kumuumiza mpenziwe

Ndani miaka 10 kwa kumuumiza mpenziwe

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAUME aliyemdunga kisu mpenziwe mara tano kwa vile alikuwa “ametalikiwa” atakula maharage miaka 10 kwa kumsababishia majeraha ya kudumu.

Robert Erick Ogeda alisukumiwa kifungo hicho na hakimu mkuu Joyce Gandani alipompata na hatia ya kumwumiza Jackline Mutindi.

Kisa na maana , Erick, alikuwa amemlaumu Mutindi kwa kuwa na mpango wa kando.

Akipitisha hukumu hakimu alisema visa vya wanaume kuwaumiza wake wao ama wapenzi wao vimeendelea kuongezeka huku akisema “wanaopatikana na hatia sharti waonje makali yake na kuadhibiwa ipasavyo.”

Mnamo Desemba 29 2018, Erick alimwinukia Mutindi na kumdunga shingo, matiti, mikono na mgongoni katika makazi yao mtaani Kabiria, eneo la Dagoretti kaunti ya Nairobi.

Baada ya kutekeleza uhalifu huo Erick alitoweka na mnamo Januari 9 2019 mkono mrefu wa sheria ulimfikia.

Alishtakiwa na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh100,000 lakini alishindwa kuilipa na kuwekwa rumande hadi Jumatano.

Akiuchambua ushahidi , Bi Gandani alisema mashahidi wote walioitwa ikiwa ni pamoja na Dkt Joseph Maundu wa Nairobi Women Hospital na muuguzi kutoka hospitali hiyo walithibitisha ni Erick aliyetekeleza unyama huo.

Kiongozi wa mashtaka Bw Jeff Musyoka aliomba mahakama ichukulie mshtakiwa hatua kali “ikitiliwa maanani alimjeruhi mpenzi wake pasipo na sababu maalum.”

Akimuhukumu Gandani, visa vya wanaume kuwashambulia wanawake wasiokuwa na silaha vimeongezeka.

Akijitetea mshtakiwa alidai kesi hiyo imechukua muda mrefu lakini hakimu akasea ni yeye aliichelewesha alipoomba baadhi ya mashahidi waitwe tena.

Mahakama ilisema siku hiyo mshtakiwa alimwuliza Mutindi mpango aliokuwa nao wa kumalizia mwaka wa 2018 lakini akamweleza anaenda kazini kisha akaongeza kumweleza , “ urafiki wao umefikia kikomo na kumtaka ashike mambo yake.”

Kwa hasira za mkizi mshtakiwa alimshika Mutindi na kumdunga kwa kisu huku akiwa amefunga nyumba.

Mutindi alipiga duru lakini hakuna mtu ambaye angeliingia ndani ya nyumba yao kwa vile Erick alikuwa amefunga kutoka ndani.

Mutindi alijinasua na kutoroka lakini akaanguka nje ya ploti na kuzirai.

Alipelekwa hospitali na msamaria mwema.

Polisi waliofika nyumbani kwa Erick waliokota kisu kilichokuwa na damu na kukiwasilisha kortini kama ushahidi.

You can share this post!

Mshukiwa wa ulaghai wa mamilioni azuiwa kusafiri

Waume walia vijana wa NYS wanawapokonya wake zao kiholela