Habari Mseto

Ndani miaka 15 baada ya DNA kuthibitisha mtoto ni wake

February 6th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MWANAMUME mmiliki wa duka la nyama alihukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani na mahakama moja ya Gichugu kwa kunajisi na kumtia mtoto mimba, baada ya uchunguzi wa DNA aliofanyiwa mtoto kudhihirisha kuwa ni wa mshukiwa.

Bw Bedan Kaburucho wa miaka 56 alidaiwa kumtia mimba mtoto wa shule katika kijiji cha Kiandai, eneo la Kirinyaga Mashariki.

Hata hivyo, mshukiwa alikuwa amepinga mashtaka alipokamatwa na kushtakiwa, na kuitaka korti kusubiri hadi mdhulumiwa azae, ndipo kipimo cha DNA kifanywe.

Alishtakiwa kwa kumnajisi mtoto huyo katika matukio tofauti kati ya Mei 1 na 31 2017.

Hakimu Mkazi Gwere Odhiambo alikubali ombi lake, lakini vipimo vilipofanywa na mtaalam wa serikali Nellie Mariam mnamo Julai 25 mwaka uliopita, matokeo yalionyesha kuwa mshukiwa ndiye baba ya mtoto msichana aliyezaliwa.

Barua ya daktari huyo iliyofikishwa kortini ilionyesha kuwa kwa asilimia 99.99, mshukiwa ndiye baba ya mtoto huyo.

Ilibainika kuwa mshukiwa alimnajisi mtoto huyo katika shamba la kahawa la familia yake, ambalo mshukiwa alikuwa amelinunua.

Mtoto huyo alieleza korti kuwa mshukiwa alikuwa akimdanganya wakati alipokuwa akitoka shuleni na kumpeleka humo shambani, wakati huo alipokuwa akilinunua shamba.