Habari Mseto

Ndani miaka 20 kwa kuua wakili kisura aliyedinda kumpa burudani

August 2nd, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MMILIKI wa kilabu cha kuuza pombe aliyemuua wakili mwenye umri wa miaka 27 baada ya kukataa wakienda kujivinjari atatumikia kifungo cha miaka 20 gerezani.

Erastus Ngura Odhiambo almaarufu Baba Billy na Ediot alisukumiwa kifungo hicho na Jaji Stellah Mutuku akisema “ ameghairi matendo yake na anastahili adhabu ya kutumikia kifungo cha gerezani.”

Jaji Mutuku alisema kuwa ripoti kutoka kwa familia ya marehemu Linda Wanjiku Irungu ambaye alikuwa anaendelea na masomo ya uzamili wa uanasheria katika chuo kikuu cha Nairobi iliomba korti iamuru anyongwe kwa vile alitamatisha maisha ya mwenda zake pasipo na sababu.

Jaji huyo alisema mshtakiwa alimuua Linda baada ya kumsaka masaa ya usiku waende kuvinjari. Alimwacha mtoto wake Billy Irungu akiwa yatima.

“ Mshtakiwa alimsaka kwa udi na ufumba Linda mara tatu baada ya kumkosa katika makazi yake. Alijihami na bastola yake akienda kwa mpenziwe na ndiyo alitumia kumuua.Amefanya mtoto waliyezaa kumkosa mama mzazi na mtu wa kumtegemea kimaisha. Alisababisha familia ya Linda kuwa na kovu ambalo halitasahaulika milele,” alisema kiongozi wa mashtaka Bi Marcel Ikol.

Bw Ikol aliomba mahakama iamuru mshtakiwa ahukumiwe kifo ili iwe funzo kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Lakini Jaji Mutuku alimuhukumu Odhiambo kifungo cha miaka 20 baada ya kumpata na hatia ya kumuua Linda. Alimpa siku 14 akate rufaa.

“ IJapokuwa mshtakiwa amejitetea alikuwa na hasira baada ya kumkosa Linda waende kuburudika angelimwacha na kushika kiguu na njia arudi katika makazi yake na marehemu angelipatwa na maafa,” alisema Jaji Mutuku.

Korti ilisema mshtakiwa alikuwa amejihami na bastola yake muundo wa Ceska alipoenda katika makazi ya marehemu usiku huo wa Desemba 11 2014.

“ Mshtakiwa alimzuia Linda kutoroka. Alimtoa ndani ya gari na kumpiga risasi kwenye bega mkono wa kulia na kumuua,” alisema Jaji Mutuku.

Alisema kuwa kosa hilo ni mbaya na sheria hutoa adhabu ya kifo lakini akasema siku hizi sheria imeipa mahakama fursa ya kuamua ikiwa mwenye hatia atatiwa kitanzi au ataadhibiwa kwa kufungwa jela.

Pia alisema mahakama imepewa mamlaka ya kusikiza malilio ya mshtakiwa na kuyatilia maanani ikipitisha hukumu.

Akijitetea kupitia kwa wakili Robert Onyango , mshtakiwa alieleza korti kwamba ni baba wa watoto wanne wa kwanza akiwa na umri wa miaka 12 na kitinda mimba yuko na umri wa mwezi mmoja unusu.

Bw Onyango alisema mshtakiwa ni mfanyabiashara aliyewaajiri wafanyakazi 13 na ndiye alindua mpango wa watumiaji wa stima kulipa kwa mtandao wa Mpesa alipokuwa ameajiriwa na kampuni ya kusambaza nguvu za umeme nchini (KPLC).

Bw Onyango pia alisema mshtakiwa alihamisha biashara yake ya kuuza pombe kutoka Buruburu hadi Karen na amewapa ajira wafanyakazi 13 na “ akihukumiwa  kunyongwa biashara hiyo itasambaratika na watoto wake wanne hawatakuwa na njia ya kujikimu kimaisha.”

Korti ilifahamishwa kuwa mke wa kwanza wa mshtakiwa alitoroka na kumwachia watoto wawili na kwamba walikuwa wamejaliwa kumpata mtoto na Linda ambaye sasa yuko na umri wa miaka mitano.

Lakini kiongozi wa mashtaka Bi Marcel Ikol aliomba korti itilie maanani mazingira ambayo mshtakiwa alimuua wakili Linda.