Kimataifa

Ndani miaka 4 kwa kumkata sikio aliyesalimia mkewe

May 2nd, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAMUME kutoka Uingereza amefungwa miaka minne jela, baada ya kumkata sikio mwanamume mwingine akitumia panga, baada ya mwanamume huyo wa pili kumsalimia mkewe.

Ajmal Mahroof alisemekana kupandwa na mori wakati alipoona mwanamume huyo akizunguumza na mkewe katika bustani moja alipokuwa akipita, ndipo akamwendea na kumuuliza kwanini alizungumza naye.

Alishtakiwa na jaji akabaini kuwa kilichofanyika kilikuwa mdhulumiwa kusalimiana na mkewe mshukiwa tu.

Kutokana na tukio hilo, mdhulumiwa aliachwa na alama ya milele, japo madaktari walifanikiwa kushikanisha sikio hilo tena.

Mahakama ya Leeds ilielezwa kuwa Mahroof alifanya vamizi hilo katika bustani ya Hyrstlands, Batley katika mji wa Yorkshire, mnamo Oktoba 17, mwaka uliopita.

Jaji Mushtaq Khokhar alisema “Kisa hiki kilitokea tu kwa kuwa hukumjua mdhulumiwa. Ni kwa kuwa tu ulimwona akizungumza na mkeo. Kilichofanyika kilikuwa tu kusalimiana.”

Kiongozi wa mashtaka Carmel Pearson alisema kuwa mpenzi wake Mahroof alikuwa akimsubiri mumewe katika bustani hiyo saa saba mchana, lakini mdhulumiwa akamtambua kama mpenzi wake rafikiye.

Alisema mdhulumiwa alimwendea mwanamke huyo kumsalimia. “Mara moja mwanamke alimwambia asisimame kuzungumza kwa kuwa mumewe angepitia hapo.”

Japo mwanamume huyo aliondoka, Mahroof alifika na kumvuta hadi katika gari lake ambapo aliingia na kutoa panga, kisha akamkata.

Japo mwanamume huyo alijaribu kumwambia kuwa alikuwa tu amemsalimia mkewe, Mahroof alimwita muongo na kusema alikuwa akizungumza na mkewe, akitaka kujua kwanini.

Baadaye alimkata sikio na vidole kisha akampiga na kukatakata sikio. Mshukiwa amewahi kufungwa kwa ajili ya kujihusisha na mambo ya kutatiza amani.

“Hili lilikuwa kosa kubwa na majeraha yalikuwa mabaya sana,” jaji Khokhar akasema.